Wednesday 29 October 2014

Chid Benzi akosa Dhamana atupwa rumande

MKALI wa Muziki wa Hip Hop nchini, Rashid Makwilo ‘Chid Benz’ jana ameswekwa rumande Segerea, kwa kushindwa masharti ya dhamana, baada ya kupandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kukutwa madawa ya kulevya, ambayo hata hivyo alikana mashitaka.
Chid Benzi, alipandishwa Mahakamani hapo majira ya saa 8 mchana akiwa amevaa suruali yake katika mtindo wa mlegezo, ambapo Hakimu Warialwande Lema, aliamuru msanii huyo atolewe nje kutokana na uvaaji huo mbaya, ili avae vizuri nguo zake na kurejeshwa kizimbani.
Akisomewa mashitaka yake na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono, alidai kwamba mnamo Oktoba 24, 2014, Chid Benz alikutwa na madawa hayo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Alidai kwamba, shitaka la kwanza linalomkabili ni kukutwa na madawa ya kulevya aina ya Heroin yenye thamani ya sh. 38,638, shitaka la pili ni kukutwa na gramu 1.72 za dawa kulevya aina ya bangi yenye thamani ya shilingi 1,720.
Mbali na hilo, shitaka la tatu ni kukutwa na vifaa vinavyotumika kuvutia dawa hizo za kulevya, ambapo alikutwa na kifuu cha nazi kitupu na kijiko kimoja.
Hata hivyo, wakili huyo alidai kwamba upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Hakimu Lema alihairisha kesi hiyo hadi Novemba 11, mwaka huu baada wadhamini kushindwa kujitokeza kwa wakati, kabla ya hakimu kutaja tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.

No comments: