Sunday 26 October 2014

Kaseja atawakimbia Yanga kama Okwi

Juma kaseja
WAKATI wowote Yanga inaweza kupoteza haki zake kwa kipa mkongwe, Juma Kaseja, baada ya klabu hiyo kushindwa kutekeleza makubaliano ya kumlipa mgawo wa pili wa fedha zake za usajili,  lakini la kushitua zaidi ni kwamba anaweza kutua Simba kwa staili kama ya Emmanuel Okwi na meneja wake amethibitisha.
Okwi alirejea Simba akitokea Yanga baada ya timu hiyo ya Jangwani kushindwa kuheshimu mkataba wake ikiwa ni pamoja na kutommalizia dau lake la usajili kwa wakati, alipogoma ndipo wakamshtaki Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) ambalo liliridhia mkataba wake uvunjwe ajiunge na timu anayoitaka ambayo ni Simba.
Kaseja ambaye ni kipa halali wa Yanga alisaini mkataba wa miaka miwili ambapo mpaka sasa ameshatumikia mwaka mmoja utakaokamilika Desemba huku klabu hiyo ikimlipa nusu ya fedha zake za dau la usajili.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa kipa huyo, Abdulfatah Saleh, alisema ameshangazwa na Yanga kushindwa kukamilisha ahadi ya malipo ya kipa huyo ambayo yalikuwa yalipwe tangu Januari 17.
Abdulfatah alisema, tafsiri iliyopo kisheria ni kwamba Yanga wamekiuka mkataba na huenda ishu ya Kaseja ikawa kama ya Emmanuel Okwi ambaye Yanga ilikiuka mkataba wake wa malipo akatua Simba.
“Unajua naweza kufananisha hili na lile la Okwi, unamuahidi mchezaji wako kumlipa fedha zake baada ya muda fulani lakini hufanyi hivyo akija kukudai unachukia, hatupendezwi na hili tunaona kama Yanga wamedhamiria kuvunja mkataba kwa kushindwa kumlipa Kaseja fedha zake mpaka sasa,”alisema Abdulfatah.
“Wakati wanamsaini tulikubaliana kwamba kiasi cha fedha kilichosalia wanapaswa kutulipa Januari mwaka huu, sasa tunazungumza huu ni mwezi Oktoba hakuna malipo yoyote, kwetu tunapata tafsiri tofauti. Angalia hata wanavyomtumia hawampi mechi za kucheza ni juzi ndiyo kacheza mechi ya kirafiki dhidi ya CDA ya Dodoma.
“Kaseja ni kipa mwenye uwezo mkubwa na hadhi yake sio kumchezesha mechi kama hizo.”
Aidha Abdulfatah alikiri kipa huyo kuhitajika na wapinzani wao Simba akisema: “Kweli Simba walionyesha nia ya kutaka kumsajili lakini hatuwezi kuzungumza nao lolote tumewaambia bado Kaseja ana mkataba na Yanga labda wazungumze nao.”

No comments: