Thursday 30 October 2014

Mdee awashauri Viongozi wa Dini waweimara

MWENYEKITI wa Taifa Baraza la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), Halima Mdee, amesema kuwa siasa za matamko ndizo zinazowapa jeuri watawala hivyo amewashauri viongozi wa dini wasimame kidete kupigania maslahi ya umma kwa vitendo.
Aidha, amesema kuwa Jeshi la polisi lilifikia hatua ya kuwapiga mabomu kutokana na Jeshi hilo kujitoa kwenye majukumu yake ya msingi na kuamua kufanya siasa kwa lengo la kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambako lilishitushwa na mapokezi makubwa wanayoyapata kwa wananchi wa kanda ya Ziwa na ujumbe mzito wanaoufikisha, jambo ambalo hawakulitarajia.
Mdee, aliyasema hayo jana wilayani Karagwe, wakati alipokuwa akifanya mahojiano maalum na kituo cha redio jamii cha Fadeco, mara baada ya kumaliza ziara wilayani humo akiwa ameambatana na Makamu wake, Hawa Mwaifunga, Katibu Grace Tendega na Naibu Katibu, Kunti Yusuh.
Alisema kuwa viongozi wa dini wamekuwa wakitoa matamko mara kwa mara wakielezea misimamo yao juu ya mambo mbalimbali yanayoedelea nchini ikiwemo umuhimu wa kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi kwenye mchakato wa Katiba, lakini watawala wamekuwa hawawasikilizi hivyo ni vema wakabadili njia ya kufikisha ujumbe.
Mbunge huyo wa Kawe, alisema kuwa suala la katiba ni la kila wananchi hivyo wabadilike waache kulalamika na badala yake wachukue hatua kwa kuhakikisha maoni yao  waliyotoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba yanaheshimiwa ikibidi kwa kufanya maandamano ya amani.
Alisema kuwa jukumu la kupigania katiba bora inayozingatia maoni ya wananchi lisiachiwe Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA ), kwani katiba ni kitu muhimu sana, ndiyo injini ya nchi na itasaidia kurekebisha mfumo wa nchi kwani kuna maeneo mengi yana utajiri mkubwa wa rasilimali lakini wananchi wake ni fukara wa kuindukia.

No comments: