Thursday 30 October 2014

Nyalandu adai Obama anamshawishi agombee Urais 2015

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amerejea kauli yake ya kwamba Serikali ya Marekani inamtaka awe mrithi wa Rais Jakaya Kikwete mwakani.
Tangu mwaka 2012, Nyalandu amekuwa akisisitiza kuwa Rais Barack Obama pamoja na uongozi mzima wa Marekani, wanataka ashike nafasi hiyo kubwa kwa kile anachosema wanaridhishwa na kipaji chake cha uongozi.
Awali, waziri huyo anayetajwa kuwa wakala wa taifa hilo lenye ushawishi mkubwa duniani, alitoa kauli hiyo kwenye hafla iliyoshirikisha watu walio karibu naye.
“Wakati huo tulidhani anatania, lakini sasa amekuwa akipita huku na kule nchini akisisitiza kuwa Rais Obama amenuia kuhakikisha yeye (Nyalandu) anakuwa Rais wa Tanzania mwaka 2015,” amesema mmoja wa watu walio karibu naye.
Akiwa mkoani Mbeya hivi karibuni, Nyalandu amenukuliwa akijipigia debe la urais kwa kusema: “Watanzania wahakikishe wanapata rais aliyeandaliwa na Mungu ili kuweza kuwavusha kutoka walipo kuelekea kwenye nchi ya neema kutokana na utajiri mkubwa wa rasilimali tulizo nazo.”
Mgombea huyo kwa sasa anakabiliwa na shinikizo linalotokana na utendaji kazi wake mbovu, amebuni mpango wa kuwapoza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kuwaandalia safari nje ya nchi.
Hata hivyo, taarifa zinasema wajumbe kadhaa wa Kamati hiyo waliokutana wiki iliyopita jijini Dar es Salaam walipinga kwa nguvu zote mpango huo, wakisema hiyo ilikuwa ‘rushwa’ ili wasiweze kuhoji utendaji kazi mbovu wa Nyalandu.
Miongoni mwa wajumbe ambao chanzo chetu kinasema walikuwa mstari wa mbele kupinga mpango huo ni Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya (CCM).
"Esther alitoa hoja nzuri sana. Alihoji iweje waziri kabla ya kuwasilisha ripoti yake kwa wajumbe aanze kuwapa ‘habari njema’ ya kuwapa safari za nje ya nchi. Wajumbe wengi waliunga mkono hoja hiyo na mwisho wa siku ikawa safari hizo zimekataliwa na wajumbe,” mmoja wa wabunge ameiambia waandishi wa habari.
Kwa upande wake, Bulaya ameulizwa na waandishi wa habari na kusema: “Siwezi kusema mengi, lakini ni kweli mjadala ulikuwa mkali.”
Ripoti ya Wizaya hiyo ambayo Nyalandu alikuwa aiwasilishe kwenye kikao hicho, ilikwama kuwasilishwa baada ya wabunge hao kuipinga wakisema ni nyepesi mno.
“Ilikuwa ripoti ya ajabu sana, ilikuwa shallow (haikuwa ya kina) sana, haikuwa na mambo mazito ambayo tulitarajia kuyaona,” alisema mjumbe mwingine.
Habari za uhakika zilisema Nyalandu alikuwa amerejea Dar es Salaam kutoka nje ya nchi saa kadhaa kabla ya kwenda kuwasilisha ripoti hiyo kwa wabunge, hatua ambayo ilionekana wazi kwamba hata yeye alikuwa hajui kilichomo.
Kama ilivyotarajiwa, Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alijaribu kumtetea Nyalandu akiwasihi wajumbe watulie wajue kilichomo. Madai yake yakawa kwamba hata kama kuna kasoro, hilo lilikuwa kosa la wasaidizi wa Waziri kwa hiyo wa kulaumiwa ni wao.
Kauli hiyo ilipingwa na wajumbe ambao walisema ilimradi ripoti hiyo inayo saini ya Nyalandu, basi yeye ndiye anayewajibika kwa upungufu wote.
Mjumbe mwingine (jina tunalo) akasema wajumbe wanataka maelezo kuhusu kashfa ya uuaji wanyamapori 704 kwa kutumia Leseni ya Rais ambayo Nyalandu alimwamuru Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori awape rafiki zake Wamarekani.
Walitaka maelezo kuhusu kashfa ya kujigawia vitalu vya miti inayomkabili Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, na walitaka kujua matumizi ya fedha zinazodaiwa kutumiwa na Nyalandu kuwahudumia wasanii anaokwenda nao ughaibuni. Matumizi ya fedha kwa ajili ya malipo ya hoteli za kitalii Dar es Salaam na Arusha; mgongano wa kiutumishi kati yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarishi, na mengine mengi.
“Ile ripoti haikuwa na kitu, ilikataliwa na akatakiwa aondoke. Ilipofika kwenye saa nne tukaahirisha kikao.  Akaondoka na wataalamu wake. Aliagizwa ajipange upya awasilishe ripoti inayolingana na uzito wa Wizara na tuhuma zinazowakabili,” kimesema chanzo chetu.
Chanzo kingine cha habari kinasema Nyalandu alisema anaandamwa kwa fitina na magazeti mawili (hakuyataja) kwa sababu ya utendaji wake wa kazi, hasa kwa kuwa amewadhibiti majangili na mafisadi. Hata hivyo, utetezi huo ulipingwa na mmoja wa wajumbe aliyehoji: “Unasema unaandamwa na magazeti kwa mambo yasiyo ya kweli! mbona magazeti yanaandika na kutoa vielelezo? Kwanini wewe usitoke ukazungumza na waandishi wa habari na wewe ukatoa vielelezo vyako vya kukanusha kama kweli ni ya uongo?
Pamoja na kubanwa kwa swali hilo, Nyalandu akaendelea kusisitiza kuwa anaandamwa kwa sababu amegusa maslahi ya mafisadi ambao amewafutia kile alichokiita 'ulaji wa rasilimali za nchi'.
Hata hivyo, Nyalandu ndiye anayehusishwa mno na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na utoro kazini. Mara nyingi amekuwa akisafiri nje ya nchi, na hata anapokuwa nchini, amekuwa akitumia muda mrefu Dar es Salaam na Arusha. Wiki mbili zilizopita, katika kuonesha ‘wizara ina waziri’ alitumia ndege kuzuru maeneo kadhaa yakiwamo ya Mbeya, Njombe, Singida, Tabora, Arusha, na Kilimanjaro. Pia alikwenda Serengeti kinyemela kupata taarifa za kuuawa kwa ndovu kadhaa.
Amejitahidi kuzima habari zinazohusu matukio ya kuuawa kwa ndovu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutaka kuuhadaa umma kwamba amefanikiwa kwenye mapambano dhidi ya ujangili.
“Hakuna habari ya kuuawa ndovu ambazo utaziona; mtasikia habari za kukamatwa pembe tu. Magazeti hayaandiki. Mitandao ya kijamii (ukiwamo mtandao maarufu nchini) haiandiki tena habari za kashfa za Nyalandu, na hata zile zilizokuwamo zimefutwa au kufungwa kabisa. Amehakikisha kila mahali anadhibiti,” kimesema chanzo chetu.
mwandishi wetu   aliripoti kwa kina juu ya Nyalandu kuwa na safari na wasanii wawili, Aunty Ezekiel na Kassim Mganga.
Licha ya Aunty Ezekiel kukanusha juu ya ziara hiyo ya kikazi ya Nyalandu, lakini Mganga kwa upande wake ameibuka na kuthibitisha kwamba safari hiyo iliratibiwa na Nyalandu.
Mganga aliyekwepa kuzungumza  Ijumaa iliyopita, siku moja kabla taarifa zake zilisomeka kwenye gazeti la HabariLeo, toleo Na. 02864 la Alhamisi ya Oktoba 23, mwaka huu.
Katika kurasa za katikati za gazeti hilo linalomilikiwa na Serikali, Mganga amesema walipelekwa Marekani na Nyalandu.
Msanii huyo aliyerejea hivi karibuni kutoka huko Ughaibuni katika tamasha aliloliita ni la kutangaza utalii wa Tanzania nchini humo, anasema ametengeneza mtandao kwa ajili ya kazi za nje.
Mganga anasema huko alifanya kazi kama ya kutoa burudani, akiwa na Msanii wa maigizo Aunt Ezekiel na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ambaye ndiye aliyewapeleka.

No comments: