Monday 20 October 2014

T.I apangawisha serengeti Fiesta 2014 Dar


TAMASHA la Serengeti Fiesta 2014, limefungwa rasmi juzi usiku katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam huku likisindizwa na burudani nzito kutoka kwa wasanii mbalimbali wa ndani na nje nchi wakiongozwa T.I kutoka Marekani.
 Shoo ya mwisho ya tamasha la Serengeti Fiesta ambalo limedhaminiwa na kinywaji cha Serengeti Premium Lager, lilivutia maelfu ya mashabiki waliofika kushuhudia nyota wa muziki kama T.I, Davido, Naseeb Abdul 'Diamond Platinum', Alikiba, Mwana FA, Stamina, Weusi na TMK wote wakitoa shoo ya nguvu.
 Katika viwanja hivyo vyaLeaders ilikuwa ni gumzo na sehemu ya pekee kwa mashabiki waliofika kushuhudia shoo ya aina yake kutoka kwa wasanii wa kimataifa.
 Waliokuwa wa kwanza kufungua shoo hiyo jukwaani walikuwa washindi wa Super Nyota wa msimu uliopita, ambao walipagawisha vilivyo mashabiki.
Wasanii wa Tanzania walistahili pongezi kwa kufanya shoo nzuri. Wasanii hao ni Mo Music, Y-Tony, Makomando, Recho, Vanessa Mdee, Barnaba, Linah, Shaa, TMK Wanaume Family, Tip Top Connection, Ommy Dimpoz na Ya Moto Band.
 Hata hivyo umati uliofurika viwanjani hapo ulipagawa zaidi, baada ya wasanii nyota kama Micharazo kupanda jukwaani na nyimbo kama Baadaye na Kimya.
 Stamina alishangiliwa zaidi baada ya kudhihirisha kipaji chake kwamba yeye kweli ni msanii bora wa miondoko ya muziki laini nchini. Wasanii wengine waliopagawisha vilivyo ni pamoja na Mwana FA, Young Killa, Weusi, Ney wa Mitego kabla ya Ali Kiba kutangaza kwa mashabiki kwamba mfalme arudi tena jukwaani. Kiba alishangiliwa na mashabiki waliokuwa wakimfuatilizia wakati akiimba wimbo wake wa Mwana Dar es Salaam.
 Kabla ya T.I kupanda jukwaani, Diamond na Davido waliwapagawisha vilivyo mashabiki na wimbo waliouimba kwa kushirikiana wa My number one remix.
 Muda uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki ni wakati msanii bora duniani T.I alipopanda jukwaani na kusababisha mashabiki kupiga makelele alipoanza kupiga shoo.
 T.I alishangaza mashabiki vilivyo wakati alipotumbuiza nyimbo kama Whatever you like, What you know, I’m never scared, Big shit poppin, Swagga like us, No mediocre na Live your Life ambazo ziliwafanya mashabiki wapige mayowe muda wote alipokuwa akitumbuiza.
 T.I aliwashukuru mashabiki na akawarudisha kidogo Afrika wakati alipoimba wimbo wa Ejeajo ambao alishirikiana na P-Square, aliendelea kuwashukuru mashabiki wa muziki wake nchini na kusema anatamani angekuja nchini kabla ya jana.
 Akizungumza na waandishi wa habari Meneja Chapa wa kinywaji cha Serengeti Fiesta, Rugambo Rodney alimpongeza T.I kwa kuonesha shoo nzuri.
 Rugambo alisema; ”Mwaka huu ziara ya Serengeti Fiesta ilikuwa na mafanikio makubwa na kwamba imeweka historia baada ya kujivunjia rekodi zake katika matamasha yaliyopita ya Serengeti fiesta nchini Tanzania.
 "Nina furaha na kwa niaba ya wenzangu, napenda kumshukuru kila mdau aliyefanikisha kufanyika kwa tamasha hili…mashabiki, wasanii, vyombo vya habari, waandaaji, hoteli na mawakala wote."

No comments: