Monday 17 November 2014

Arsenal yamnyatia Peter Cech

Peter Cech
Arsenal wamepanga kumchukua kipa wa Chelsea, Petr Cech katika dirisha la Januari.
Kipa huyo wa kimataifa wa Czech amepoteza namba yake kwa kipa kinda wa Ubelgiji, Thibaut Courtois aliyerejea klabuni hapo baada ya kumalizika mkopo wa misimu mitatu akikipiga Atletico Madrid ambapo alifanikiwa kulishawishi benchi la ufundi la Chelsea kuwa anastahili kucheza mbele ya Cech.
Na sasa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger atatoa dau la Pauni 7 milioni kwa ajili ya kumnasa kipa huyo, ambaye amekiri kutokuwa na furaha na maisha ya benchi Stamford Bridge na anataka kuondoka.
Inadaiwa kuwa mabosi wa Chelsea pamoja na kocha wao, Jose Mourinho hawatakuwa na kipingamizi kama kipa huyo ataamua kujiunga na timu yoyote pinzani katika Ligi Kuu ya England kama ilivyofanya kwa Juan Mata wakati alipojiunga na Manchester United Januari mwaka huu.
 Liverpool, Manchester United, Paris Saint-Germain na Real Madrid zote zinadaiwa kumnyatia kipa huyo mkongwe, lakini inadaiwa kuwa mwenyewe anataka kubakia London ambako familia yake imekuwa ikiishi kwa miaka 10 sasa.
Cech ana mkataba na Chelsea mpaka mwaka 2016 na imeripotiwa kuwa Wenger yuko tayari kumpatia mkataba wenye mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki kama ule anaochota kwa sasa Stamford Bridge.
Hivi karibuni Cech alitoboa siri kwamba anachukia kukaa benchi Chelsea na kuna mpango akaondoka kwa ajili ya kutetea nafasi yake katika timu ya taifa ya Cezch.
“Sijaongea na mtu yeyote, lakini nadhani wananijua vizuri sana klabuni kiasi cha kufahamu kuwa hali haipo kama ambavyo ningeweza kufikiria,” alisema kipa huyo.
“Euro (2016) ikiwa njiani na timu ya taifa ikiwa akilini, hakuna muda wa mimi kukaa katika benchi na kutocheza. Kama hali haitabadilika kwangu, nitatoa suluhisho,” alisema kipa huyo.
Chelsea ilimsajili Cech kutoka Rennes ya Ufaransa Julai 2004 kwa dau la Pauni 7 milioni ambalo kwa wakati huo lilimfanya awe kipa ghali zaidi katika historia ya Chelsea.

No comments: