Tuesday 4 November 2014

Chadema ya Kusanya Milion Tisa kwa saa moja

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetumia muda wa saa moja kukusanya zaidi ya Sh9 milioni.
Chama hicho kilikusanya kiasi hicho cha fedha katika saa moja tangu kuzindua Programu ya Siasa Mtandaoni, iliyofanyika jana jijini humo na kilizindua vipengele vitatu, kikiwamo cha uchangishaji fedha kutoka kwa wananchi ili kukisaidia katika harakati za kuikomboa Tanzania huru.
“Zaidi ya Watanzania milioni 20 wanatumia simu za mkononi hapa nchini. Tunaomba watumie simu hizohizo kuichangia Chadema kutekeleza majukumu yake. Vodacom wako tayari na tutaanza nao leo wakati tukiwasubiri Airtel na Tigo, ambao wataanza Jumatano ijayo.
Mfumo huu wa kuchangia utakuwa na uwezo wa kutunza kumbukumbu za wote waliochangia na kama watapenda kuonekana au la wataweza kufanya hivyo,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mifumo mitatu iliyozinduliwa jana ni malipo kwa njia ya mtandao (e-payment), kujisajili uanachama kwa njia ya mtandao (e-membership) na upataji wa taarifa za chama kupitia simu ya mkononi (Chadema media) ambayo inahitaji mhusika kujiandikisha.
Hatua hiyo inaifanya Chadema kuwa chama cha kwanza nchini kuleta mapinduzi ya teknolojia kwenye siasa.
Uzinduzi huo ulifanyika saa 5 usiku, huku uchangiaji ukipewa kipaumbele, ambapo Mbowe alitoa maelekezo kwa Watanzania wote waliokuwa wakilifuatilia tukio hilo kupitia runinga zao.
Mara baada ya maelekezo kutolewa, wachangiaji walikuwa wengi hata kusababisha mfumo kuelemewa kutokana na idadi hiyo kuzidi uwezo wake.
Uchangiaji ulikuwa mkubwa ndani ya dakika kumi za mwanzo, huku ukipungua kadri muda ulivyozidi kwenda.
Katika dakika nne za mwanzo zaidi ya Sh4.7 milioni zilichangwa, kiwango ambacho kiliongezeka kufikia zaidi ya Sh6.798 milioni katika dakika ya 8 na dakika moja baadaye tayari kulikuwa na zaidi ya Sh7.6 milioni.
Hadi sherehe hizo zilipohitimishwa na viongozi wa kitaifa wa chama hicho kuondoka ukumbini saa 6:00 usiku, michango hiyo kupitia Mpesa ilikuwa imefikia Sh9,262,041.
Baada ya uzinduzi huo, chama hicho kilianza kupokea michango kutoka kwa marafiki na wanachama wa mikoani pamoja na vyama rafiki vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi na jumla ya Sh56.42 milioni pamoja na Dola700 za Marekani zilikusanywa.

Wachangiaji hao walipata nafasi ya kushikana mikono na mwenyekiti wa chama pamoja na viongozi wengine ambao ni Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed.
“Hatuupendi umaskini, lakini tunawapenda maskini wote wa nchi hii. Waliopo madarakani wameupaka rangi umaskini na kila asemaye kuwa ni mtoto wa mkulima anaonekana anafaa. Haya ni matusi kwa wakulima wa nchi hii kwa kuwa kinachowakwamisha ni sera mbovu zilizowekwa na watungaji hao ambao hawana uchungu na maisha ya watu wa chini,” alisema Mbowe.

No comments: