Friday 14 November 2014

Kampuni za Simu zinaibia watanzania

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amekiri kwamba kuna tatizo katika kampuni za simu nchini la kuwaibia wateja wao.
Makamba alikiri hilo jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji.
Haji alisema wizi huo si mkubwa kama uliofanyika kwenye Escrow, bali ni wizi mdogo ambao wateja wanaibiwa Sh2,000 au 3,000 katika simu zao.
“Mpemba wa Konde akiibiwa Sh3,000, Mnyamwezi aliopo Tabora akiibiwa 2,000 ukizijumlisha ni mamilioni wanaibiwa Watanzania,” alisema.
Alihoji Serikali inafikiriaje kuhusu gharama za kwenda kutoa malalamiko yao katika Mamalaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA).
Pia alitaka kufahamu ni nani aliopo nyuma ya pazia hilo au CCM ina fungu katika wizi huo?
Akijibu, Makamba alisema CCM haihusiki na wizi huo unaotokana na kampuni za simu na kwamba chama hicho ni kizuri, makini na kimekuwa kikiaminiwa na wananchi.
“Napenda nikiri dhahiri tatizo la wizi na dhuluma lipo na ni kubwa na ndio zilisababisha tukaweka kanuni na hatua za kuchukua katika kudhibiti wizi huo,” alisema.
Pia alisema wateja wa vijijini hawawezi kufuatilia madai yao hadi Dar es Salaam, hali ambayo imeifanya Serikali kuanzisha kituo cha kushughulikia malalamiko hayo.
“Sheria inazitaka kampuni kuweka huduma kwa wateja, lakini wakati mwingine utaratibu huo una matatizo, unaweza kupiga simu hazipokewi, unaweza ukaambiwa usubiri lakini wakati ukisubiri unakatwa,” alisema.
Alisema katika kituo walichokianzisha, kutakuwa na namba ya bure ya kupiga simu, hali itakayomrahisishia mteja kusafiri hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kulalamika.
Alisema kituo hicho kitakuwa wazi saa 24, mteja atapewa namba atakapotoa lalamiko lake ili lishughulikiwe.Alisema kama lisiposhughulikiwa itakuwa sababu ya kampuni kuchukuliwa hatua.

No comments: