Wednesday 26 November 2014

Kenya yaitaka dunia kuingilia machafuko ya kisiasa nchini Somalia

Kenya imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati mgogoro wa kisiasa ndani ya uongozi wa Somalia, ambao umeathiri amani ya kanda hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na naibu rais wa Kenya William Ruto alipokuwa na mazungumzo na naibu waziri mkuu ambaye pia waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Slovakia Miroslav Lajcak. Amesema tofauti zilizopo kati ya rais Hassan Sheik Mohamud wa Somalia na waziri mkuu Abdiweli Ahmedi zinarudisha nyuma juhudi za nchi za kanda hiyo kuleta utulivu nchini humo. Naibu Ruto amesema wana wasiwasi na mpasuko kati ya viongozi hao wawili, na kwamba hali bado ni tete ndani ya nchi hiyo.
Waziri mkuu wa Somalia Ahmed, Oktoba 25 aliripotiwa kutangaza uamuzi wa kuvunja baraza la mawaziri bila kushauriana na rais. Hata hivyo rais Mahmud baadaye alipinga mabadiliko hayo na kumfukuza kazi Ahmad kwa "kutoa uamuzi wa kufedhehesha" na kutangaza kitendo cha kuvunja baraza la mawaziri ni batili, pia aliwataka mawaziri walioondolewa kuendelea na kazi zao kama kawaida.

No comments: