Saturday 8 November 2014

Mbowe afichua ufisadi bomba la gesi mtwara

Mbowe afichua ufisadi mzito bomba la gesiMWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Taifa, Freeman Mbowe, amefichua tuhuma za ufisadi wa kutisha akisema kuwa gharama ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam imeongezwa maradufu huku kiasi kilichoongezwa kikiwa ni hongo kwa viongozi wa serikali na jamaa zao.
Katika madai hayo aliyoyatoa juzi jioni katika Uwanja wa Barafu mjini Igunga na kurejea jana Uwanja wa Parking Nzega mjini, Mbowe amesema kuwa ufisadi huo unahusisha viongozi wa Serikali ya CCM, ndugu zao wa kifamilia na maswahiba katika biashara.
Alisema kuwa, ufisadi huo umewashtua hata nchi wahisani ambao Tanzania imekuwa ikiwategemea katika bajeti za kuendesha shughuli za maendeleo, akiongeza kuwa hata utegemezi huo ni dalili ya matokeo ya ufisadi na kutowajibika.
Mbowe ambaye jana alizindua rasmi operesheni ya chama hicho inayoitwa ‘Operesheni Delete CCM’ (ODC), ikiwa inakiandaa chama hicho kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, Kura ya Maoni ya Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu mwakani, ameitaka Serikali kuwajibika katika hilo.
Akizungumza kwa msisitizo kuhusu tuhuma hizo, huku akirejea kashfa mbalimbali kubwa ambazo zimekuwa zikihusishwa na Serikali ya CCM, Mbowe alisema kuwa kashfa hiyo ya sh trilioni 2 ambazo ni fedha za mkopo zitakazolipwa na Watanzania maskini, imevunja rekodi.
“Ndugu wananchi, Watanzania wenzangu…tumekuwa tukilia na ufisadi katika nchi hii. Wizi kila mahali, kila siku chini ya Serikali ya CCM. Tulilia sana na ufisadi wa EPA, ufisadi wa EPA ulikuwa mkubwa kweli kweli, leo kila mtu anajua kuwa tunalia na ufisadi wa Akaunti ya ESCROW, ni ufisadi mkubwa kweli kweli zaidi ya EPA…
“Kwenye ufisadi huo wa ESCROW, wamehongwa watu huko serikalini huwezi kuamini. Ufisadi wa bilioni 200…karibu kila mtu amehongwa, wakiwemo watu wakubwa kabisa, ndiyo maana unaona wanahangaika wote. Sasa kuna ufisadi mwingine umefanywa, ESCROW mtaiona ni cha mtoto.
“Mnajua ule ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam…sasa pale jamaa wamepiga kweli kweli, safari hii si mabilioni tu, wamepiga trilioni. Tukiwaambia trilioni wananchi wa kawaida mnaweza msielewe. Ngoja niwafafanulie kwa urahisi mjue namna zilivyo fedha nyingi,” alisema Mbowe.
Akifafanua tuhuma hizo kuhusu kashfa hiyo ilivyotokea, Mbowe alisema kuwa gharama halisi za ujenzi wa bomba hilo zilikuwa ni Dola za Marekani milioni 600, ambazo zilipaswa kulipwa kwa kampuni inayohusika na kandarasi hiyo kutoka China.
“Wananchi wakati mwingine unaweza kusumbuka kuamini haya mambo yanayofanywa na viongozi wa Serikali ya CCM…gharama ya ujenzi wa bomba hilo imeongezwa na wakubwa mara mbili ya gharama halisi, wakubwa wamechukua yote waliyoongeza na sasa mradi huo utakuwa ni Dola za Marekani milioni 1200, kutoka milioni 600,” alisema Mbowe.
Kiongozi huyo ambaye kesho anaingia siku ya tatu ya ziara hiyo ya ODC (Operesheni Delete CCM), akiwa bado yuko mkoani Tabora, alisema kuwa fedha hizo Dola za Marekani milioni 1200 ni fedha za mkopo ambazo Tanzania imekopa, hivyo zitalipwa kwa jasho la Watanzania maskini ambao hawajui namna fedha zao zinavyotafunwa, huku Serikali ikionekana haina fedha kwa shughuli muhimu za maendeleo ya wananchi.

No comments: