Tuesday 25 November 2014

Mwakezaji ajeruhi watu 6 kwa risasi zanzibar

Zanzibar. Jeshi la Polisi Zanzibar linamshikilia mwekezaji kutoka Ufaransa, Ivan Kodeh kwa tuhuma za kuwajeruhi watu sita wakiwamo waandishi wa habari kwa risasi baada ya uongozi wa Hoteli ya Cristal kudaiwa kugoma kukabidhi madaraka kwa uongozi mpya huko Paje, Mkoa wa Kusini Unguja.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI), Salum Msangi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa tano asubuhi katika hoteli hiyo.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni waandishi wa habari, Munir Zakaria wa Channel Ten na Kuruthum Ali wa TBC ambao walikuwa kazini. Wengine ni Ramadhani Mohammed (25), Wadi Ame Khamis (35), Ashraf Suleiman (36) na Nadir Ali Juma (28).
Alisema mwekezaji huyo anashikiliwa pia kwa kumiliki silaha inayodaiwa kutumika katika shambulio hilo aina ya Gamo yenye namba 04-4L-720/70-07 ambayo imetengenezwa Hispania.
Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 6 (3) cha Sheria ya Silaha namba 2 ya mwaka 1991 na Kifungu namba 19 cha Sheria ya Silaha Tanzania Sura ya 223, mtu yeyote akiwa Tanzania na Zanzibar haruhusiwi kutumia au kumiliki silaha pamoja na risasi. Alisema taratibu za kumfikisha mahakamani zimeanza.
Katika tukio jingine, Msangi alisema polisi pia inamshikilia raia wa Poland, Artur Miarka (52) kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya BSA air Rifle na risasi zake pamoja na darubini ya kumsadia kuona mbali.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa katika eneo la Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja na baada ya kuhojiwa alisema amekuwa akitumia silaha hiyo kwa muda wa miaka mitatu Visiwani hapa.
Alisema kutokana na matukio hayo, polisi imetoa wiki moja kwa wawekezaji wote wanaomiliki silaha Zanzibar kuzisalimisha katika vituo vya polisi kabla ya kuanza kwa msako katika hoteli zote Unguja na Pemba.

No comments: