Thursday 27 November 2014

Sakata la Siti Mtevu lafika mbali

Hatima ya kashfa ya kudanganya umri inayomkabili aliyekuwa mrembo wa Tanzania mwaka 2014, Sitti Mtemvu bado ipo kizani baada ya polisi kuikana kauli ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita)
Rita, kwa upande wao ilieleza wiki moja iliyopita kuwa imekabidhi polisi vielelezo kuhusu uchunguzi wa kashfa hiyo kwa lengo la kuchukua hatua.
Jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alikana kupokea taarifa za vielelezo hivyo vilivyotumiwa kuombea cheti cha kuzaliwa cha Sitti Mtemvu.

Wiki mbili zilizopita, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ilijivua lawama katika kashfa hiyo na kuiachia Rita.
Akizungumza  jana, Kova alisema, “Jeshi la Polisi halijapokea vielelezo vyovyote kutoka Rita, wamepeleka wapi? Iwapo waliviwasilisha katika kituo chochote cha polisi watoe taarifa iliyo sahihi, iwapo vielelezo hivyo vitatufikia tutachukua hatua stahiki,” alisema Kova.

Kwa upande wao, Rita waliahidi kuwasilisha vielelezo hivyo wiki hii na kwamba vilicheleweshwa kutokana na kukamilisha upekuzi wa taarifa za kuombea cheti pamoja na cheti cha awali kilichokuwa kikitumiwa na Sitti Mtemvu.

Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Rita, Emmy Harrison alisema jana kuwa idara yake imekamilisha taratibu zote zinazotakiwa na vielelezo hivyo vitakabidhiwa rasmi polisi.
“Haya ni masuala ya kisheria, hivyo sisi tumeshakamilisha kile tulichotakiwa kukifanya na mchakato huu bado unaendelea, tupo katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kuripoti polisi, wiki hii vielelezo vya Sitti vitapelekwa kwenye vyombo vya usalama kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema Harrison.

No comments: