Wednesday 26 November 2014

Uwanja wa ndege mjini Tripoli washambuliwa

Ndege za kivita za jeshi la Libya jana zilishambulia uwanja wa ndege wa Mitiga huko Tripoli na kusababisha safari zote za ndani na nje ya nchi kusitishwa.
Kamanda wa jeshi la anga Brigedia Saqr Jeroshi amesema shambulizi hilo lililenga kukikatia usambazaji wa vifaa kikundi cha kigaidi cha Libya Dawn, na kuongeza kuwa anga za magharibi na mashariki za Libya sasa zinalindwa na ndege za jeshi la taifa.
Aidha amesema mbali na uwanja wa ndege wa Mitiga, bandari za Sirte, Misrata na Zuwarah zinaweza kuwa sehemu nyingine zitakazolengwa kushambulia wapiganaji wa kiislamu. Mitiga ni uwanja wa ndege pekee unaofanya kazi, baada ya kundi la Libya Dawn kuharibu uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tripoli na kuudhibiti mwezi Agosti. Muungano wa wanamgambo wa kiisalamu umeweka utawala wake ili kupambana na ule unaotambulika kimataifa, ambao sasa upo uhamishoni mji wa mashariki wa Tobruk.

No comments: