Friday 14 November 2014

Yanga na Simba waja kivingine

Wakati Yanga wakiwapa mapumziko ya siku 10 nyota wake kabla ya kurejea kuanza maandalizi rasmi ya mechi ya ‘Nani Mtani Jembe 2’, wapinzani wao, Simba, wamewapa mapumziko ya siku 14 huku wakitamba kikosi chao kuwa ‘fiti’ tayari kwa mchezo huo.
Timu hizo zinatarajia kushuka Uwanja wa Taifa, Desemba 13, kuwania taji la ‘Nani Mtani Jembe 2’ linaloratibiwa na wadhamini wakuu wa timu hizo, bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ikiwa ni mara ya pili tangu kuanzisha kwa kampeni hiyo.
Hadi jana, Simba ilivuna Sh17,900,000 dhidi ya Sh 62,100,000 za Yanga huku Novemba 11, Simba ikiwa nazo Sh 20,115,000 dhidi ya Sh59,885,000 za Yanga na Novemba 10, Simba Sh20,445,000, huku Yanga wakivuna Sh 59,555,000.
Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema wao wameishaanza maandalizi ya mchezo huo, lakini si rasmi
Alisema wao wataanza kuyafanyia kazi baada ya nyota wao kurejea toka mapumziko ya siku kumi baada ya ligi kusimama kupisha michuano ya Chalenji.
“Vijana wetu tumewapa mapumziko ya siku kumi, na wakirejea maandalizi yanaanza kwa ajili ya Mtani Jembe 2, tuna imani tutafanya vyema katika mchezo huo,”alisema Njovu.
Ofisa habari wa Simba, Humphrey Nyasio alisema kikosi chao mara baada ya ligi kusimama kimepewa mapumziko ya wiki mbili, ambapo wanatarajia kurejea Novemba 21 kuanza maandalizi ya ‘Nani Mtani Jembe2’.
Alisema baada ya kurejea vijana wao wataendelea na maandalizi yao kama kawaida, huku akili zao zikiwa kwa ‘Nani Mtani Jembe 2’ , mashindano ambayo wao ni mabingwa watetezi wa kampeni hiyo baada ya mwaka jana, kuwabugiza Yanga mabao 3-1.
Aliwataka mashabiki kuiunga mkono kwa wingi klabu yao katika kampeni hiyo, hasa katika kuvutana ili wazoe fedha zote, yaani Sh 95milioni na kumwachia mtani (Yanga), Sh 5milioni pekee na kwamba watarajie mabao matatu msimu huu.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe aliwataka mashabiki Simba wavutane zaidi ili kuipatia timu yao fedha kwani hadi sasa wanazidiwa na Yanga.

No comments: