Wednesday 17 December 2014

Mwanafunzi afia gesti akitoa Mimba

Wanafunzi wakielekea Shule
MWANAFUNZI  wa kidato  cha tatu katika shule ya Sekondari ya Tongoni nje kidogo ya jiji la  Tanga,  (jina tunalihifadhi) amekutwa amekufa ndani ya nyumba ya kulala wageni alikopelekwa kutolewa mimba bila mafanikio.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe mwanafunzi huyo alikutwa amekufa juzi katika nyumba ya kulala wageni iliyopo barabara ya 21 jijini Tanga.
Mmoja wa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema kwamba mwanafunzi huyo aliingia saa 4.00 asubuhi siku ya tukio akiwa ameambatana na kijana mmoja wakakodi chumba.
“Baadaye alikuja mwanaume mmoja wa makamo ambaye alituuliza kama wameingia mwanafunzi huyo na mwenzake, tulipomwonyesha chumba  walichoingia naye akakodi chumba cha jirani ndipo tukaona wote wakijifungia kwenye chumba kimoja,” alisema mhudumu.
Mhudumu huyo alisema baada ya muda wa saa moja, mvulana na mzee huyo wakaaga kwamba wanatoka huku wakisema kwamba msichana amebaki chumbani akiwa amepumzika. Akithibitisha habari hizi, Kamanda Massawe alisema taarifa ya tukio hilo ilitolewa na mhudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni katika Kituo cha Polisi cha Chumbageni Jijini Tanga.
“Tatizo ni kwamba nyumba hii ya wageni wahudumu wake hawakuwapa wageni hao daftari ili waorodheshe majina yao hivyo inakuwa vigumu  kuwafahamu,” alisema Kamanda Massawe na kufafanua kuwa alifariki akitolewa mimba ya mwezi mmoja.
Kamanda Massawe alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na kifo hicho.

No comments: