Friday 30 January 2015

Kiongozi wa Makaburu aachiliwa Huru Afrika Kusini

Eugene Alexander de Kock
Kiongozi wa zamani wa utawala wa kiimla wa makaburu nchini Afrika Kusini na ambaye alikuwa kinara wa kuongoza kitengo hatari cha kuwatesa watu weusi, Eugene de Kock, amesamehewa, kuhurumiwa na kuondolewa gerezani.
Eugene Alexander de KOCK alikuwa akitumikia hukumu ya mauwaji na mateso kwa wakereketwa wengi wa chama cha ANC, lakini sasa waziri wa haki na sheria Nchini Afrika Kusini, Michael Masutha, amesema kuwa de Kock ameachiwa huru kwa manufaa ya umoja wa kitaifa.
Alikuwa ametubu mbele ya tume ya haki na maridhiano kwamba alikuwa amesababisha zaidi ya vifo vya watu mia moja na pia kuhusika katika vitendo vya kuwatesa watu kinyama na ufisadi, hasa akiwalenga waliokuwa wakipinga utawala wa ubaguzi wa rangi.
Kanali huyo wa zamani wa polisi aliyekuwa na mataji mengi mno alisamehewa kwa mengi ya makosa aliyofanya, lakini akazuiliwa gerezani kwa makosa dhidi ya binadamu kabla ya kufungwa jela maisha.
Tarehe ya kuachiwa huru kwake kwa sasa bado ni siri.

No comments: