Saturday 31 January 2015

Matola aachia madaraka Simba

Klabu ya Simba imethibitisha kuachana na kocha msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola na kueleza kumweka hadharani mrithi wake atakayesaidiana na kocha mkuu, Goran Kopunovic wakati wowote kuanzia sasa.
Mapema jana, Rais wa Simba, Evance Aveva alieleza kupokea barua ya kujiuzulu kwa Matola na kubainisha kuwa katika barua hiyo, Matola ameeleza kutingwa na majukumu ya kifamilia hivyo hawezi kuendelea kuinoa Simba kama kocha msaidizi.
Alipotafutwa na gazeti kuzungumzia uamuzi wake huo, Matola alitaka aulizwe vizuri Aveva ndiye alitolee ufafanuzi suala hilo na si yeye kwani tayari ameachana na klabu hiyo.
Hata hivyo, kocha huyo alionekana kupoteza mvuto kwa baadhi ya mashabiki ambao mara kadhaa wamekuwa wakimshinikiza ang’atuke Simba.
Kwa mujibu wa Aveva, Simba imepokea barua ya kujiuzulu kwa kocha huyo juzi ikiwa ni siku moja baada ya Simba kuruhusu kipigo cha magoli 2-1 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa.
Pia, Aveva amekiri jahazi la timu yao kuendelea kuzama kutokana na kutoka sare mfululizo na kupoteza mechi mbili kwenye ligi na kuwa timu ya nne kutoka mwisho na pointi 13 katika mechi 11 ilizocheza.
“Ni kweli timu yetu inakwenda mrama, matokeo tunayopata hayaridhishi hata kidogo, kama uongozi tulikutana na benchi la ufundi kuhusu hali ya timu yetu ambao wametuambia ni kutokana na ratiba ya ligi kuwabana.
“Leo, kocha Goran Kopunovic anatimiza siku 30 tangu alipoanza kuinoa Simba, katika kipindi hicho ameiongoza Simba kucheza mechi kumi na kwa uwiano katika kila siku tatu wanacheza mechi moja.
“Kwa hali hii, timu inachoka, wenzetu Yanga na Azam walitolewa mapema, hivyo kupata muda zaidi wa kujiandaa tofauti na sisi ambao tumecheza hadi mwisho,” alisema Aveva.
Akizungumzia mpasuko katika klabu yao, Aveva alisema hawana mpasuko wowote na sasa wanajipanga ili kuhakikisha timu yao inarejesha makali kwenye ligi kwa kushirikiana pamoja na kuwataka mashabiki kuwa na subira.

No comments: