Monday 12 January 2015

Pinda asema kauli yake ya "wapigeni " alimaanisha amani

Neno “piga” lina maana ya “fanya kitendo cha kukutanisha vitu kwa nguvu, fumua, ezeka, zaba, shambulia, chapa na tandika” kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Oxford, lakini kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda neno “wapigeni” lilimaanisha “kuendelea kulinda amani”.
‘‘Baada ya kutoa kauli  hiyo  kuna watu wakaeleza kuwa sasa Waziri Mkuu analeta sera za kupiga. Hapana ilikuwa kujaribu kukemea watu wasileta fujo kama kwamba Serikali iko likizo,’’ alisema Pinda.
Alisema akiwa bungeni aliwahimiza Watanzania  kuilinda amani na utulivu  uliopo nchini kwa gharama yeyote ile na iwapo atatokea mtu kutaka  kuivunja amani hiyo, hatapewa nafasi badala yake atashughukiwa kwa namna yeyote.
Waziri Pinda alitoa kauli hiyo tata mwaka jana wakati wa kipindi alichokianzisha bungeni cha mswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, baada ya kluulizwa kuhusu vitendo vya polisi kupiga rais badala ya kuwafikisha mahakamani.
Kauli yake ilisababisha wanaharakati kumjia juu na wengine kutaka kwenda mahakamani kutokana na kwenda kinyume na misingi ya utawala bora.
Waziri Pinda alitoa tafsiri ya neno hilo alipoongea na wananchi wa Mkoa wa Katavi wakati akihitimisha ziara yake kwa kukutana na wananchi wa Tarafa ya Kabungu,  Kata ya Mpanda Ndogo wilayani Mpanda.
Alisema amani iliyopo hapa nchini ni ya miaka mingi iwapo wakitokea watu wanaotaka kuleta chokochoko, watashughulikiwa tu.
Akizungumzia wakimbizi walioko mkoani Katavi ambao wanatarajiwa kupewa uraia, alisema ni lazima mkoa ujiandae kuwapokea raia hao wapya na hiyo nayo ni changamoto  kubwa kwa mkoa.
‘‘Wakimbizi hao wanaotarajiwa kupewa uraia ni wengi kwani ni zaidi ya 120 na changamoto kubwa  iliyo mbele ya mkoa. Hivyo ni vyema utaratibu mzuri ukaandaliwa kwa ajili ya kuwapokea raia hao wapya na mkoa umejiandaa vizuri utalifanyia kazi suala hilo kuhakikisha amani iliyopo  inatunzwa,” alisema.
Alisema mbali ya wakimbizi hao walioko makazi ya Mishamo wapo wakimbizi wengine walioko kwenye makazi ya Katumba ambao nao wanakaribia kufikia  80,000 ambao pia watapewa uraia.

No comments: