Tuesday 13 January 2015

Tambwe ashuhudia ajabu la mwaka

MFUNGAJI Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, straika Amissi Tambwe, amesema haelewi tatizo ni nini, lakini yaliyomtokea kwenye mechi mbili za mwisho za Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi ni maajabu kwake.
Tambwe amemaliza michuano hiyo bila kuwa na bao, lakini akasema hatasahau mechi hizo.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mrundi huyo ambaye aliifungia Simba mabao 19 katika msimu uliopita wa ligi, alisema siyo jambo geni kwake kupoteza nafasi za kufunga, lakini nafasi ambazo amezipoteza katika mechi dhidi ya Shaba na JKU hatazisahau.
Tambwe alisema hajui nini kilitokea wakati akimalizia nafasi ambazo alikuwa akizipata uwanjani kwani hali hiyo haijawahi kumtokea tangu atue nchini.
“Sijui nini kimenitokea, sijawahi kukosa mabao ya namna hii, nafasi kama hizi ndiyo siku zote nimekuwa nafunga nimejishangaa sana kwa kweli,” alisema Tambwe.
“Siku zote nimekuwa sitaki kujiamini kupita kiasi ili niweze kufunga, lakini nilivyofanya hadi nikakosa sijui nini kimetokea, acha tu ndio mpira.”
Tambwe alikosa kufunga akiwa katika nafasi nzuri katika mechi ya makundi dhidi ya Shaba ambayo Yanga ilishinda bao 1-0, pia alishindwa kufunga dhidi ya JKU katika robo fainali juzi Alhamisi walipofungwa bao 1-0.

No comments: