Monday 12 January 2015

Yanga yamtibulia Mzungu wa Simba

KUPIGWA chini kwa Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi mjini hapa kumetibua mambo mawili.
Kwanza waandaaji wanalia kwamba mapato yataporomoka, lakini kocha wa Simba, Goran Kopunovic, amesema atabadili mbinu zake kuanzia leo Jumamosi.
Amesema watakomaa kwa kutumia nguvu kubwa kuhakikisha kwa namna yoyote ile wanafanya kilichoishinda Yanga na Azam ili kulinda heshima ya timu, mashabiki na hata kibarua chake.
Ikohivi; Azam FC iliondoka Zanzibar jana Ijumaa asubuhi baada ya kutolewa katika Kombe la Mapinduzi wakati Yanga wakijipanga kuondoka leo Jumamosi, lakini kuondolewa kwa timu hizo zilizopewa nafasi ya kutwaa ubingwa kumemshtua kocha wa Simba, Kopunovic, ambaye ametangaza mapambano.
Azam ilitangulia kutupwa nje katika hatua ya robo fainali kwa kufungwa penalti 7-6 na Mtibwa Sugar mapema juzi Alhamisi kabla ya Yanga kukumbana na kipigo cha bao 1-0 mbele ya JKU.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kopunovic, alisema kutolewa kwa Azam na Yanga kumemshtua na sasa amewageukia wachezaji wake akiwaambia hakuna kudharau chochote. Alisema hakufikiria kama timu hizo zinaweza zisifike nusu fainali na sasa atauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo wao wa leo usiku dhidi ya Polisi ya Zanzibar.
Alisema wataingia uwanjani katika nusu fainali hiyo wakiwa na fikra kwamba wanakutana na timu iliyomng’oa bingwa mtetezi KCCA ya Uganda.
“Mpira ni mchezo wa makosa, Yanga walitengeneza nafasi nyingi jana (juzi) lakini wakashindwa kuzitumia, ni tatizo linaloweza kutokea hata kwetu, nimeshawaambia wachezaji wangu tutaingia kwa akili moja ya kutengeneza nafasi na kuzitumia,”alisema Kopunovic.
“Hakuna aliyetarajia mambo yaliyotokea jana (juzi), hili ni kama somo kwetu kwamba tukifanya makosa nasi tutakwenda na maji.”
Katika nusu fainali nyingine, Mtibwa itacheza na JKU.
Mapato yaporomoka
Kutolewa kwa Yanga kumetibua mipango ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kwani kilitarajia kipate fedha nyingi kwa mapato ya milangoni.
 
Mashabiki na wadau wa soka wakiwemo viongozi wa soka visiwani hapa, wengi wao walitarajia Yanga ingetinga fainali huku wakiipa nafasi ya kucheza na Simba na kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na viingilio.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA, Ally Bakari, alisema: “Ni kweli kuondolewa kwa Yanga kwenye michuano hii ni hasara kwetu kwani ndiyo timu pekee iliyokuwa ikiongoza kuingiza mashabiki wengi uwanjani, inayofuatia ni Simba.
“Kuna hasara kubwa itapatikana baada ya michuano hii, ukiangalia tangu ianze mechi za Yanga ndiyo zilikuwa zinaongoza kuwa na mashabiki wengi ikifuatiwa na Simba.
“Hivyo wengi walikuwa na imani kwamba Yanga na Simba zitakutana fainali na mapato yangepatikana mengi, lakini imekuwa kinyume.
“Mashabiki wamekuwa wengi uwanjani kila inapocheza Yanga kwa kuwa timu hii haijashiriki Kombe la Mapinduzi kwa miaka miwili, hivyo mashabiki wao wa hapa walikuwa na hamu ya kuiona timu yao inafika fainali, hii ni hasara kubwa kwa waandaji pamoja na ZFA ambao ndio wasimamizi wa soka hapa visiwani.”
Leo Jumamosi, Simba itacheza na Polisi wakati Mtibwa Sugar itacheza na JKU katika nusu fainali ikiwa ni mara yao ya pili kukutana kwenye mashindano haya, awali walikutana katika hatua ya makundi na kutoka sare ya bao 1-1.

No comments: