Thursday 21 May 2015

Kumbukumbu za miaka 19 ya ajali ya MV Bukoba yaadhimishwa leo

Kumbukumbu ya miaka 19 ya ajali ya meli ya Mv. Bukoba iliyopoteza maisha ya abiria zaidi ya 800 katika ziwa victoria baada ya kuzama na kupinduka mei 21 mwaka 1996, imefanyika leo katika makaburi ya pamoja yaliyoko eneo la Igoma nje kidogo ya jiji la Mwanza, huku baadhi ya wananchi waliopoteza ndugu zao kwenye ajali hiyo wakiitaka serikali kupitia mamlaka ya udhibiti usafiri wa nchi kavu na majini ( SUMATRA ) kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya usafiri wa majini.
Viongozi wa madhehebu ya dini ya kikristo na kiislamu walianza tukio hilo kwa kuwakumbuka wapendwa wao kwa sala na dua.
 
Miongoni mwa watu waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo mbaya ni pamoja na mwanamitindo wa kimataifa Flaviana matata ambaye alishindwa kujizuia kutokwa machozi wakati alipokuwa akisimulia tukio la kumpoteza mama yake mzazi, huku mfanyakazi wa shirika la maendeleo la taifa ( NDC ) Stewart Alphonce pamoja na msanii wa muziki wa Hip hop nchini Joseph Haule maarufu kama Profesa J, wakisema hali ya usafiri katika ziwa victoria bado ingali tete.
 
Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza ambao walihudhuria kumbukumbu hiyo wameiomba serikali kuitangaza tarehe 21 mei kila mwaka kuwa ni siku ya maombolezo ya kitaifa ili kuwakumbuka wahanga waliopoteza maisha yao kwenye ajali ya meli ya Mv.Bukoba.
 
Serikali katika tukio hilo la kumbukumbu ya miaka 19 imewakilishwa na katibu tawala wa wilaya ya ilemela Ramla Bakari Juma

No comments: