Saturday 23 May 2015

Mwalimu akutwa na viungo vya albino

Polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga inawashikilia watu watano, akiwamo mwalimu wa shule ya msingi na mwanamke mmoja, kwa tuhuma za kukutwa na viungo vya albino wakiwa katika harakati za kutaka kuviuza wilayani Nzega na Kahama.

Tarifa ya kamanda wa polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Jastus Kamgisha iliyotolewa kwa waandishi wa habari mjini hapa jana na Mkuu wa polisi wilayani hapa, Leonard  Nyandahu, watu hao walikamatwa saa 7:00 mchana katika nyumba moja ya kulala wageni inayofahamika kwa jina la Maji Hoteli iliyopo Phantom, Kata ya Nyasubi.

Nyandahu alimtaja mwalimu huyo kuwa ni Bahati Kirungu (56) anayefundisha katika Shule ya Msingi ya Katungulu iliyoko Kata ya Wendele na mwanamke anayeitwa Regina Kashinje (40) ambaye ni mkulima na mkazi wa Isagehe, Nzega.

Wengine ni Mhoja John (24) mkulima na  mkazi wa Isagehe Nzega, Bilia Busanda (39) mkulima na mkazi wa Mogwa Nzega, Shija Makandi (60) mkulima na mkazi wa Isagehe Nzega na Aboubakary Ally (25) ambaye ndiye  mtunza siri ya watu hao ambaye ni mkulima na mkazi wa Isagehe Nzega.

 Nyandahu alidai kuwa Mei 19, asubuhi, mkuu wa upelelezi wa kituo cha polisi wilayani Nzega alipata taarifa kuwa kuna mtu anauza viungo vya albino, ndipo walipoweka mtego. Hata hivyo, alidai kuwa walishindwa kuwakamata na baadaye mtu huyo alihamishia biashara hiyo wilayani Kahama.

Nyandahu alisema maofisa upelelezi wa Tabora kwa kushirikiana na ofisa upelelezi wa Kituo cha Polisi cha Kahama, walifuatilia nyendo za watu hao na wakaweka mtego mwingine wa kuwakamata uliofanikiwa  kuwanasa.

Hata hivyo, polisi wilayani Kahama wanaendelea kuwashikilia watu hao kwa mahojiano zaidi ikiwa ni pamoja na kuubaini mtandao wao.

Kukamatwa kwa watu hao kumekuja wakati Serikali ikiwa katika mikakati ya kudhibiti mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambao wameanza kusakwa tena mwaka huu baada ya vitendo hivyo kutulia kwa muda mrefu.

No comments: