Monday 11 May 2015

Nyota watatu kutemwa Simba

SimbaTIMU ya Simba imepanga kuwatema nyota wake watatu na kusajili wachezaji wenye uzoefu ili kuimarisha kikosi hicho ambacho kinaundwa na chipukizi wengi.
Simba imeanza mikakati ya usajili kwa ajili ya msimu ujao baada ya kumaliza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa nafasi ya tatu huku ubingwa ukinyakuliwa na watani wao wa jadi Yanga na Azam kushika nafasi ya pili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi Ofisa Habari wa timu hiyo, Haji Manara, alisema uongozi unasubiri ripoti ya kocha wa timu hiyo Mserbia, Goran Kopunovic, ili zoezi la usajili liweze kufanyika kwa kufuata mapendekezo yake.
Alisema pamoja na Simba kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu, bado wanaamini wachezaji wao wana viwango na ubora unaokubalika hivyo hawana mpango wa kufanya mabadiliko makubwa kwa ajili ya msimu ujao.
Alisema ripoti ya Kopunovic inayotarajiwa kukamilika mapema wiki hii, ndiyo itatoa mwongozo kwa Kamati ya Usajili ya Simba inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Zacharia Hans Poppe kama wachezaji watakaoongezwa ni wa kulipwa au wazawa.
“Wapenzi wa Simba wasitarajie mabadiliko makubwa katika usajili kwani timu hii itaendelea kuwepo na wachezaji watakaoachwa hawawezi kuzidi watatu na watakaosajiliwa itategemea mapendekezo ya kocha,” alisema.
Wakati huo huo, Kopunovic alielezea kufurahishwa na ushindi walioupata wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku akidai matokeo hayo yamedhihirisha ubora wa kikosi hicho kwa msimu huu.
Alisema wachezaji walicheza kwa kujituma na kumfanya ajivunie kikosi bora licha ya kuzidiwa mbinu na watani wao wa jadi, Yanga na kushindwa kutwaa ubingwa msimu huu.
Simba iliyomaliza ligi kwa kujikusanyia pointi 47 imekosa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika mwakani baada ya kuzidiwa kete na Azam iliyomaliza kwenye nafasi ya pili.

No comments: