Thursday 14 May 2015

Tindu Lissu achafua hali ya hewa bungeni

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu jana alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kudai kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ni ya kichovu, kauli ambayo ilizua mabishano makali kati yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama.
Akichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2015/16, Lissu alisema Serikali hiyo imeshindwa karibu kila jambo, ikiwamo uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Alisema uchovu huo pia umejidhihirisha wazi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kueleza kwamba mpaka sasa haijapewa fedha za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, wakati imebaki miezi mitano ufanyike.
Lissu alivutana na Spika Anne Makinda pale alipotakiwa kukaa chini kumpisha Mhagama azungumze baada ya kugoma kwa maelezo kuwa waziri huyo ameingilia wakati akitoa ufafanuzi wa uchovu wa Serikali.
Mvutano huo ulianza Lissu alipokuwa akisema kuwa mbali na kukwama kwa uandikishaji katika Daftari la Wapigakura, hata katika upigaji wa kura za kupitisha Katiba Inayopendekezwa katika Bunge Maalumu la Katiba, marehemu, mahujaji na wagonjwa ni miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo waliopiga kura.
“Hata Uchaguzi Mkuu mpaka sasa Serikali haijatoa fedha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hakuna maandalizi yoyote. Hatukubali kuona Serikali hii ikijiongezea muda kwa kisingizio hicho,” alisema Lissu.
Kauli hiyo ilimwinua Mhagama na kueleza kuwa katika Bunge la Katiba zilipigwa kura halali, huku akifafanua jinsi Serikali ilivyofanya shughuli nyingi za maendeleo.
“Mheshimiwa Spika, Lissu analidanganya Bunge. Kauli zake ni za kuudhi namwomba asiendee kupotosha umma,” alisema Mhagama huku Lissu akisisitiza kauli yake.
Wakati Mhagama akisimama kuomba utaratibu wa Spika, Lissu naye alisimama akipinga kitengo cha kukatizwa na waziri huyo kuchangia, tukio ambalo liliingiliwa na Spika na kuzua majibizano.
“Huyu ananizuia kwa misingi gani, kafuata utaratibu upi,” alisema Lissu huku Mgahama naye akiendelea kuzungumza huu akiwa amesimama kabla ya wote wawili kukatishwa na Spika Makinda aliyewataka wakae chini na kufafanua kuwa yeye ndiye anayejua utaratibu.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Makinda alimpa nafasi Mhagama kuendelea kuzungumza na alipomaliza alimpa nafasi Lissu ili amalizie kuchangia hotuba hiyo.
Mbowe

Awali, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliwasilisha hotuba ya kambi hiyo, akisema hakuna maandalizi yoyote yanayofanywa na Serikali ambayo yanaashiria wazi kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba mwaka huu.
Mbowe ambaye pia hakumaliza kusoma hotuba yake baada ya kukatishwa na Spika wa Bunge, Makinda baada ya kuibuka ubishi juu ya muda wa uwasilishaji, alisema hayo wakati akitoa maoni ya kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alisema ukweli huo umethibitishwa na NEC kwenye ukurasa wa randama ya Tume hiyo namba 13 unaosema: “Kwa upande wa maandalizi ya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu, 2015 Tume hatujapokea fedha hadi sasa.”
Alihoji kama Serikali haijaipatia Tume fedha kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, inategemea miujiza gani kuwa ifikapo Oktoba uchaguzi huo utafanyika.
“Ni lini zabuni zitatangazwa kwa ajili ya makandarasi mbalimbali ambao watasambaza vifaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na tarehe ya kuwapata hao wazabuni ni lini?” alihoji.
Alisema wakati Serikali ikishindwa kuipatia NEC fedha kwa ajili ya kufanya maandalizi ya uchaguzi ili ufanyike katika mazingira ya amani, haki na utulivu, imeamua kuwekeza na kujiandaa kupambana na wananchi wake.
“Hii ni kutokana na ukweli kuwa tuna taarifa kuwa Serikali imeamua kuagiza zaidi ya magari 777 kwa ajili ya Jeshi la Polisi, kuanzia yale ya maji ya kuwasha, doria na shughuli za ukaguzi katika mwaka huu wa fedha,” alisema.
Alisema NEC inadaiwa madeni na makandarasi ambao walisambaza vifaa kwenye uchaguzi uliopita ambayo yanathibitishwa kwenye randama ukurasa wa 13, lakini hazikutengwa kwenye bajeti
Kura ya maoni
Mbowe alisema Sheria ya Kura ya Maoni ya Mwaka 2013, iliweka bayana muda maalumu wa kuchapisha swali la kura ya maoni, kutoa elimu kwa umma na siku ya kufanyika kwa kura ya maoni na kuwa muda wa kufanya yote hayo kwa mujibu wa sheria umeshapita.
“Haiwezekani tena kwa kura ya maoni kufanyika sasa au baadaye bila kwanza sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 kuletwa bungeni.”
CHANZO: MWANANCHI

No comments: