Tuesday 16 June 2015

Ajali yaua 23 huko Mafinga Iringa

Mkuu wa wilaya ya Mufindi, Mboni Mhita akiwatembelea majeruhi hospitali ya Wilaya mjini Mafinga (Picha na Frank Leonard).

WATU 23 wamekufa katika ajali iliyohusisha basi na lori mjini Mafinga, Iringa huku wengine 34 hali zao zikiwa mbaya.
Ajali hiyo imetokea miezi mitatu baada ya ajali nyingine ya basi kuua zaidi ya watu 50 katika eneo la Changarawe, mjini Mafinga.
Ajali hiyo iliyohusisha basi mali ya Kampuni ya Another G Trans lenye namba za usajili T 927 CEF na lori aina ya Scania, mali ya Kampuni ya Bravo Logisticts ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyopatikana, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 1.45 usiku katika eneo la Kinyanambo A, barabara kuu ya Iringa- Mbeya.
Kwa mujibu wa mashuhuda wamesema basi hilo liligongana uso kwa uso na lori hilo lenye namba za usajili T 916 AQM likiwa na tela namba T 965 BEH.
Akizungumza na wanahabari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Pudenciana Protas alisema; “Wakati basi hilo lenye uwezo wa kupakia abiria 65 likiwa linatokea Iringa kuelekea Njombe, lori hilo lililokuwa likiendeshwa na Rogers Wales mwenye miaka 39, Msambaa mkazi wa Mwanza lilikuwa likitokea barabara kuu ya Mafinga kuelekea Iringa.”
Protas alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo, Nicholas Magula (30) aliyekosa umakini na kutaka kulipita gari lingine bila kuchukua tahadhari.
Alisema miili ya marehemu na majeruhi hao ilikimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi ya mjini Mafinga, mapema baada ya ajali hiyo kutokea.
Alisema miili 12 ya watu waliokufa imekwishatambuliwa na kuwataja kuwa ni pamoja na Lucas Pancras, Blasto Samila, Dickson Luvanda, Albert Silla (askari wa Ruvu JKT), Eva Mbalinga, Khadija Mkoi (4), Clemence Mtati, Mohammed Lalika, Castory Mwakiamba, Damiana Myala na Silo Nziku ambao wote walikuwa katika basi hilo na dereva wa lori, Rogers Wales.
Alitaja majeruhi wa ajali hiyo waliokuwa katika basi hilo kuwa ni pamoja na Emma Lupembe (35), Veronica Simba (20), Shafia Ally (24), Mariam Mbise (23), Anita Makwela (24), Benitha Sagara (18), Bertha Mkoi (27), Rahel Mavika (18),, Selina Fulgensi (23), Maria Mwenda (17), Ndipako Mbilinyi (28), Alexander Mkakazi (28), Meshack Kibiki (44), Simoni Jumbe (22), Jerry Lutego (36), Enock Kanyika (18) na Yusuph Lulandala (22).
Wengine ni Deogratias Kayombo (21), Petro Mwalongo (21), Paul Chahe (21), Kennedy Msemwa (28), Emanuel Anthony (21), Mode Shilazi (21), Godfrey Kanyika (39), Boniface Bosha (20), Ambiana Meshack (35), Martha Kanyika (30), Melika Tonga (2.5), Yusuph Luhumba (34) na Damiana Kuyala (42).
Protas alisema majeruhi wengine wanne, wanaume wawili na wanawake hawajatambuliwa majina yao kwa sababu walikuwa hawaongei.

No comments: