Monday 22 June 2015

Ali Kiba atangaza Bifu na Diamond

Brighton Masalu
VITA! Saa chache tu baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar akitokea nchini Marekani kwa shughuli za kimuziki, staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ametangaza kile kinachotafsirika kuwa ni vita dhidi ya hasimu wake kwenye anga la muziki huo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ijumaa Wikienda lina ‘full’ stori.
Ali Kiba alitema cheche Alhamisi ya wiki iliyopita ndani ya Hoteli ya Sea Cliff, Masaki jijini Dar, kulikokuwa na uzinduzi wa kampeni ya kupinga vita ujangili, iliyoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, huku akiwa ni mmoja wa mabalozi sanjari na mlimbwende wa zamani, Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi ‘K-Lyin’.

Baada ya shamrashamra za ‘event’ hiyo, haraka sana kama mshale wa Mmakonde, mwandishi wetu alimfuata Ali Kiba, lengo kuu likiwa ni kusikia chochote juu ya ushindi wa Tuzo za Kili ambapo alizoa tano binafsi na moja ya kushirikishwa.
Kiba alisema anaamini alistahili kushinda tuzo zote kwani vigezo na sifa anazo na amejiandaa kikamilifu kupambana na yeyote anayedhani kuwa ni mfalme wa muziki huo.

Katika mahojiano hayo, mwandishi wetu alimkumbusha Ali Kiba uwepo wa Diamond ambapo kwa haraka sana alimkata kauli mwandishi kwa kusonya na kuweka wazi kuwa miongoni mwa mambo ambayo humpa kichefuchefu, ni pamoja na kusikia jina la Diamond likitajwa mahali popote penye uwepo wake!

“Kaka, sitaki kabisa kulisikia jina hilo, linanipa kichefuchefu, unajua kwa kipindi ambacho nilikaa kimya, nilikuwa nausoma mchezo lakini hakuna aliyeweza kuchukua kiti changu na kuamua kurejea ulingoni kwa kishindo na kuanzia sasa hivi ni mapambano mwendo mdundo,” alisema  Kiba na kuongeza:

“Simaanishi kuwa hakuna msanii mzuri kama mimi, naomba nisieleweke vibaya, wapo lakini siyo huyo dogo (Diamond), muziki ni zaidi ya mbwembwe, niko kikazi na sasa nimedhamiria kweli, kama anaamini yuko fiti, kazi zitaweka wazi ukweli na si drama za kitoto.”

 VIPI KUHUSU YEYE NA WEMA?
Mwandishi wetu alitaka kujua kulikoni msanii huyo alimuweka Wema Sepetu kwenye ukurasa wake wa Instagram akimmwagia shukrani lukuki na si mtu mwingine?

“Wema amekuwa ni shabiki wangu wa siku nyingi mno, alianza kunipenda kupitia wimbo wangu wa Hands Across the World (kwenye Project ya One-Eight) na kuanzia hapo amekuwa akinipa sapoti kubwa sana, siwezi kukaa naye mbali eti kisa huyo jamaa (Diamond).

“Naamini kwa asilimia nyingi sana hata huu ushindi wangu wa tuzo, umechangiwa na sapoti yake pamoja na wadau wangu wengine,” alisema Kiba.

Pia, mwandishi wetu alimtaka staa huyo kufafanua madai ya kutoitendea haki video ya Wimbo wa Mwana, ambapo alisema, watu wengi walitarajia aifanye kulingana na mawazo yao ndiyo maana akaamua afanye vile anavyoaamini ingekuwa bora.

“Kila mtu alikuwa ameshatengeneza picha ya jinsi video ya wimbo itakavyokuwa, halafu sifanyi kazi kwa kushindana na mtu, ndiyo maana ilionekana tofauti na mawazo ya wengi, namalizia kwa kusema salamu zimfikie jamaa (Diamond) kuwa mapambano ndiyo kwanza yameanza,” alisema Kiba.
Diamondi nae afunguka *Hadi tunakwenda mitamboni, jitihada za kumpata Diamond aweze kuzungumzia vita hiyo iliyofufuka upya hazikuzaa matunda kufuatia simu ya staa huyo aliyekuwa nchini Afrika Kusini kikazi, kuita bila majibu.

 TUJIKUMBUSHE

Kwa muda mrefu sasa, Kiba na Diamond wamekuwa wakiripotiwa kuwa na bifu la chini kwa chini linalotokana kugombania ufalme wa muziki Bongo.

No comments: