Wednesday 17 June 2015

Lowasa ashtumiwa kucheza Rafu

BAADHI ya watangaza nia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameituhumu kambi ya Edward Lowassa kuwa imeanza ‘kucheza rafu’ katika mchakato wa kutafuta wadhamini unaoendelea hivi sasa ndani ya chama hicho.
Watangaza nia hao waliozungumza nasi wamedai kwamba wapambwe wa Lowassa wanakusanya na kuondoka na kadi za wanachama wa chama hicho waliojitolea kumdhamini.
Kwa mujibu wa taratibu za ndani ya CCM, watangaza nia wanatakiwa kupata wadhamini 450 katika walau mikoa 15 ya Tanzania; ukiwa ni wastani wa wadhamini 45 kwa kila mkoa, lakini wapambe wa Lowassa wamekuwa wakichukua wadhamini wengi zaidi.
Mkoani Mwanza pekee, kambi ya Lowassa ilidai kwamba ilipata jumla ya wadhamini 1600, katika 45 wanaotakiwa, lakini Ukomboz blog haijathibitisha kama kadi za uanachama za wadhamini wote hao nazo zilichukuliwa.
Taarifa zaidi zinabainisha kwamba timu hiyo imekuwa ikihakikisha inapata idadi kubwa ya wadhamini kuliko ile iliyopangwa na kuhodhi kadi za wanachama wa chama hicho ili kupunguza kasi yao katika kudhamini watangaza nia wengine.
Mmoja wa watangaza nia ambaye gazeti hili halitamtaja kwa sasa, amedai kuwa kwa vile kila mwanachama hatakiwi kudhamini mtu zaidi ya mmoja, zinapochukuliwa kadi nyingi inamaanisha kwamba watangaza nia nyingine watapata taabu kupata wadhamini kwa sababu wanachama walio hai si wengi.
 limeelezwa kuwa hali hiyo ya watu kuondoka na kadi za wanachama ilijitokeza zaidi katika Jiji la Mwanza na hata Zanzibar, na zaidi ya hapo, mipango kama hiyo imekwishatayarishwa mkoani Mara, ambako mtoto wa Baba wa Taifa, Makongoro Nyerere, Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ndiko wanakotoka.
Kutoka Zanzibar, taarifa hizo zinabainisha kwamba Lowassa na wafuasi wake, walidhibitiwa katika mpango wao wa kutaka kudhamiwa kwa idadi kubwa ya wanachama.
"Alilenga kuonekana anaungwa mkono kwa nguvu zaidi Zanzibar . Huku Zanzibar hatukuruhusu kabisa suala hilo lifanyike na tukatii utaratibu wetu wa kutaka kila anayetaka kudhaminiwa apate wanachama 45," kilieleza chanzo chetu ndani ya CCM visiwani humo.
Lakini timu yake hiyo ikiwa kisiwani Pemba, inadaiwa kukusanya kadi za wanachama, baadhi zikidaiwa kuwa na vitambulisho vya kupiga kura na kisha kuondoka navyo.
Mtangaza nia huyo aliyezungumza na gazeti hili alisema kwa tabia ya kukusanya wadhamini wengi kupita mahitaji, wapo wagombea wanaoweza kuja kupata shida ya kupata wadhamini katika maeneo kama Pemba ambako CCM haina wanachama wengi.
Juhudi za kumpata Msemaji wa Lowassa, Elizabeth Missokia, kuhusu tuhuma hizi hazikufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni.
Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Oganaizesheni), Muhammad Seif Khatib, alisema chama kitahakikisha wagombea wote wanapata idadi hiyo ya wadhamini inayotakiwa.
Tayari Makamu Mwenyekiti wa CCM – Tanzania Bara, Philip Mangula, amezungumzia mwenendo wa mchakato wa kutafuta wadhamini kwa watangaza nia wa chama hicho, mapema wiki hii, akisema kila anachofanya mwana CCM anayetafuta wadhamini 450 kitaingia katika kumbukumbu zitakazotumika wakati wa kufanya tathmini kwa ajili ya mchujo.
Mangula amekwishaagiza kamati za maadili za wilaya kukutana mara baada ya watangaza nia kujaza majina ya wadhamini wilayani na muhtasari upelekwe mara moja makao makuu ya CCM.
Alisema muhtasari huo utakapofikishwa makao makuu CCM utatumiwa na kamati ya maadili ngazi ya taifa katika kufanikisha tathimini kwa kila mgombea.
Hayo yanatokea wiki kadhaa tangu CCM kutangaza rasmi ruksa kwa wanachama wake kutangaza ratiba ya uchukuaji fomu za kuwania kuteuliwa kugombea urais miongoni mwa wanachama wake.
CCM kilitangaza uamuzi wake huo Mei 24, mwaka huu. Kwa mujibu wa chama hicho, watangaza nia watatakiwa kuheshimu kanuni na misingi ya chama hicho na ni marufuku kwa kwao kufanya mbwembwe, ikiwa ni pamoja na kukodi watu kwa ajili ya kushangilia wakati wa kuchukua fomu au kurudisha.
Mwongozo huo wa CCM uliwekwa bayana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, fomu ya kugombea urais ilianza kutolewa Juni 3, mwaka huu na kuzirudisha Julai 2, mwaka huu saa 10 jioni.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba katika mwaka huu, idadi ya wadhamini imeongezeka kutoka 250 hadi 450, huku idadi ya mikoa ya kutoa wadhamini hao nayo ikiongezeka kutoka 10 hadi 15.
Katika taarifa yake hiyo, Nape alibainisha sababu ya kuongeza kwa wadhamini kuwa ni idadi ya wanachama wa CCM kuongezeka na wakati huo huo idadi ya mikoa vile vile kuongezeka.
“Lazima wagombea waende kwenye mikoa hiyo, ambapo mikoa 12 kwa Tanzania Bara na mikoa mitatu Zanzibar na moja ya mkoa uwe Pemba au Unguja,” alisema Nape kwa wakati huo na kuongeza; “Wakati wa kuchukua fomu na kurejesha ni marufuku mgombea kufanya mbwembwe za aina yoyote, ni muhimu wagombea kusoma kanuni na kuzielewa mapema.”
Nape alisema Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM itachuja majina ya wagombea urais Julai 8, mwaka huu, Kamati Kuu (CC), itachuja majina Julai 9, mwaka huu na Halmashauri Kuu nayo itapitisha jina la mgombea urais Zanzibar, wakati jina la mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litapitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu Julai 11, mwaka huu mjini Dodoma

No comments: