Wednesday 17 June 2015

Mahakama yamfutia adhabu ya kifo kwa kiongozi wa kigaidi

MAHAKAMA moja nchini Misri imemfutia adhabu ya kifo Adel Habara ambaye ni mkuu wa kundi moja lenye silaha nchini humo.

Shirika la Habari la Anadolu la nchini Uturuki limeripoti habari hiyo ambapo limesema kuwa mahakama moja ya rufaa nchini Misri ilitangaza kufutiwa kwa adhabu hiyo juzi Jumapili.

Kufutiwa kwa adhabu ya kifo kwa kiongozi wa kundi hilo la wanamgambo wa Ansar al Jihad la Rasi ya Sinai kumeambatana na kuachiliwa kwa wanachama wengine sita wa kundi hilo kutokana na rufaa waliyokata.

Abdel Habara na wenzake hao sita wanakabiliwa na mashtaka ya kuendesha operesheni ya mauaji inayojulikana kwa jina maarufu la Mauaji ya Pili ya Rafah.

Wanachama 35 wa kundi hilo akiwemo mkuu wake walitiwa mbaroni mwaka 2013 baada ya kuuawa maafisa 25 wa usalama wa Misri huko Rafah.

Wiki mbili zilizopita, mahakama ya Rufaa ya az Zaqaziq ya Misri ilitoa adhabu ya kifo kwa wanachama wanane wa makundi yenye silaha ya Rasi ya Sinai.

Miongoni mwa watu hao alikuwemo Adel Habara ambaye alikuwa na tuhuma za kuua askari 25 wa Misri akiwa yeye pamoja na wenzake.

No comments: