Saturday 20 June 2015

Mwakyembe aibua mapya kwenye mbio za urais CCM

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe ameibua mapya wakati akichukua fomu ya kuwania nafasi ya urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinzudi (CCM).
Dk Mwakyembe, ambaye hivi karibuni aliibuka katika vyombo vya habari, akisema kuna watu wanamchafua kupitia mitandao na kuapa kuwatafuta na kuwafikisha mahakamani, kazi hiyo ameifanya na matokeo yake ameyatangaza jana.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu katika Makao Makuu ya CCM, Dodoma jana, Dk Mwakyembe alisema watu waliokuwa wakimchafua mitandaoni na kumgombanisha na wagombea wenzake, wamekamatwa akiwamo kijana ambaye yuko kwenye kundi la mmoja wa mgombea urais, ambaye hakumtaja jina.
Mapya Amesema mmoja wa vijana hao, amekiri kufanya hivyo huku akieleza dhamira yao ya kutaka kuihariri ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu tuhuma za Richmond na kuisambaza upya.
“Jambo la kuambiwa nina chuki na mtu limekuwa likinishtua na kuniumiza sana, lile suala (Richmond) lilikuwa ni uamuzi wa Bunge. “Juzi nilipokuwa Burundi nikaambiwa mimi namtukana mtu mitandaoni, kwamba nitapambana kufa kupona, kuhakikisha hachaguliwi kupeperusha bendera ya CCM, niliugua baada ya kusikia,” alisema Dk Mwakyembe.

Alifafanua kuwa kutokana na kutokuwa na tabia ya kumtukana mtu mitandaoni, aliamua kwenda Polisi Kitengo cha Uhalifu wa Mitandaoni ili amjue anayefanya vitendo hivyo. Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, alifanikiwa na alizungumza na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaamu, Kamishna Suleiman Kova na kumuomba amsaidie kuhakikisha watu hao wanapatikana.
Dk Mwakyembe hakuishia kwa Kova, amesema alikwenda Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambapo nako walimsaidia na kufanikiwa kukamata baadhi ya watu ambao ni wahusika.
Mgombea huyo alisema, atahakikisha watu hao waliohusika kumchafua wanafikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua stahiki huku akipongeza kitengo hicho kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya.
“Kijana huyo ambaye ni mfuasi wa mmoja wa wagombea urais alinishtua sana aliposema moja ya mikakati yao ni kuikarabati ripoti ya Richmond na kuisambaza upya, nilimwambia kijana wangu utafungwa na kuozea jela,” alisema.
Hakuna suluhu
Alisema, mtu aliyehusika katika sakata la Richmond ni kaka yake na anamheshimu sana lakini yeye alifanya kazi aliyotumwa na Bunge ambalo lilimwamini na kumpa kazi hiyo.
Mwakyembe alisema, hana msalie mtume na anapopewa kazi anaifanya kwa usahihi na uaminifu na kutoa taarifa bila kujali aliyehusika ni kaka yake, ndugu yake, rafiki, mke, wala mtoto.
“Huo ndio utaratibu wangu katika utendaji wa kazi, sitegemei kuficha maovu ndivyo nitakavyokuwa hata nikiwa Rais,” alisema.
Hata hivyo, alisema hana sababu ya kumchukia mgombea mwenzie kwani wanaCCM wote ni ndugu na akiteuliwa atakuwa tayari kumuunga mkono ili kwa pamoja wapeperushe bendera ya CCM.
Vipaumbele, sifa
Akizungumzia vipaumbele vyake kama atapata fursa ya kupeperusha bendera ya CCM, kwa upande wa rushwa alisema, atapambana nayo kikamilifu kama ambavyo amekuwa akifanya katika nyadhifa mbalimbali.
“Ninayafanya hayo kwa kuwa nimeruhusiwa na viongozi wangu kufanya hivyo, isingekuwa hivyo nisingefanya,” alisisitiza. Sambamba na hilo alisema, atasimamia ilani ya chama chake katika utendaji wake wa kazi, ikiwa ni pamoja na kuendeleza mambo makubwa na mazuri yaliyofanywa katika uongozi wa Awamu ya Nne naye akiwa mmoja wao.
Sifa zake
Kuhusu sababu za kuwania urais, alisema alifikia uamuzi huo kutokana na sababu kuu tatu; moja ikiwa ni kuwa mwanachama wa CCM mwenye haki kikatiba na kidemokrasia ndani ya chama.
Nyingine ni kutoa wigo mpana kwa chama kumtafuta mmoja wao kati ya waliogombea hata wakiwa 100, ili apatikane wa kupeperusha bendera ya CCM.
Sababu ya tatu ni kwamba yeye ni sehemu ya Serikali ya Awamu ya Nne, mwenye uelewa mkubwa katika changamoto na mafanikio yaliyopatikana ikiwemo kipaumbele katika ngazi zote nchini.
Alisema hakuna sababu ya wanaCCM kuingia kwenye uchaguzi huu wakiwa wanyonge, kwani yeye kutoka sakafu ya moyo wake, anaamini wataingia kwenye uchaguzi wakiwa kifua mbele kutokana na mambo makubwa waliyofanya.
Dk Mwakyembe anakuwa waziri wa 10 kuchukua fomu ya kuwania urais, ikiwa ni sawa na asilimia 37 ya mawaziri wa Serikali ya Jakaya Kikwete.
Mawaziri wengine waliomtangulia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro.
Kwa upande wa manaibu mawaziri waliojitokeza kuchukua fomu ni wawili, ambao ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia, January Makamba.

No comments: