Wednesday 17 June 2015

Rais Kikwete; Napendezwa na Wingi wa wagombea

Rais Jakaya Kikwete na Linda Thomas- Greenfield(kushoto)RAIS Jakaya Kikwete ameelezea kufurahishwa na wingi wa wagombea waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, akisema ni jambo zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika chama hicho.
Aidha, amesema pia msururu wa wagombea hao ambao sasa wamefikia 36, ni uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio na kwamba kinyume cha hapo, wengi wasingependa kujihusisha nacho.
Pamoja na kufurahishwa huko, ameendelea kusisitiza kuwa, yeye binafsi hana mgombea urais anayempendelea kwa sababu wagombea wote ni wa kwake na wa chama chake, isipokuwa anayo kura moja tu ambayo ataitumia mwezi ujao wakati wa vikao mbalimbali kuamua nani awe mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Rais Kikwete amesema hayo usiku wa kuamkia juzi mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakati akizungumza na Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika, Linda Thomas- Greenfield.
Viongozi hao wawili walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton Covention Centre, Johannesburg, Afrika Kusini uliomalizika jana.
Mwanzoni tu mwa mazungumzo hayo, Linda alimwuliza Rais Kikwete: “Mheshimiwa Rais, je unaye mgombea yeyote ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea?”
Rais Kikwete alimjibu: “Sina mgombea ninayempendelea, wagombea wote ni wa kwangu, ni wa Chama changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za haki katika Chama chetu nitaitumia katika vikao mbalimbali.”
Kuhusu kile kinachoitwa utitiri wa wagombea, Rais Kikwete alisema wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM. “Hiki ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili kwa nafasi nani awe mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa sababu ya wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka ya karibuni. Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha mafanikio yetu katika miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu wangeogopa kujitokeza kugombea nafasi hiyo.”
Aidha, Rais Kikwete alisema hana tatizo na kujitokeza kwa wagombea wengi wa nafasi ya urais zamu hii kupitia CCM kwa sababu huwezi kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa sababu ni haki yao.
Alisisitiza wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika chama hicho na uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio.

No comments: