Wednesday 17 June 2015

TFDA Dodoma yateketeza bidhaa feki za Mil. 20/- za Kitanzania

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati imeteketeza bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu zenye thamani ya Sh. milioni 20.
 
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa kazi ya uteketezaji jana mjini hapa, Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Kati, Fredrick Luyangi, alisema bidhaa zilizoteketezwa zina uzito wa tani 4.4.
 
Luyangi alisema bidhaa hizo ni dawa tani 0.44, chakula tani 3.08 na vipodozi uzito wa tani 0.93.
 
Aidha, TFDA imewaonya wafanyabiashara kuacha kuuza bidhaa zisizofaa, zilizoisha muda wa matumizi na pia vipodozi vyenye viambata vilivyopigwa marufuku baada ya kuonekana kuwa vina sumu.
 
"Wafanyabiashara wote wanatakiwa kuzingatia kanuni na sheria ili wauze dawa, vyakula na vipodozi vinavyofaa kwa matumizi ya binadamu," alisema.
 
Aliongeza vilevile kuwa wananchi wanapaswa kuepuka matumizi ya vyakula, dawa na vipodozi ambavyo vimeisha muda wake na ambavyo havijasajiliwa nchini.

No comments: