Tuesday 16 June 2015

Vijiji 14 wilayani kahama vinakabiliwa na ukosefu wa huduma ya Afya.

Zaidi ya vijiji 14 wilaya ya kahama mkoani Shinyanga  vinavyouzunguuka mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu vinakabiliwa na ukosefu wa huduma bora za afya kwa muda mrefu na hivyo kusababisha wananchi kufuata huduma hiyo kwa umbali wa zaidi ya kilometa 75 huku waathirika wakubwa wa hali hiyo ni kinamama wajawazito na watoto.
Vijiji hivyo vya kata za Bugarama,Bulyanhulu na Mwingiro vyenye zaidi ya wakazi 47,000, wananchi wamekuwa wakiwaomba bila mafanikio  viongozi mbalimbali kushughulikia tatizo hilo ambalo limekuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa afya zao. 
 
Wakizungumza na ITV baadhi ya wananchi wa kata za Bugarama na Bulyanhulu wamesema bado tatizo hilo la ukosefu wa huduma bora za afya limekuwa likiwasumbua kwa kiasi kikubwa  licha ya kuwepo kwa zahanati moja ambayo haikidhi mahitaji hususani ya ongezeko la watu huku kinamama wajawazito wakipata usumbufu mkubwa katika kutafuta huduma za upasuaji zinapohitajika.
 
Aidha katika kusaidia kukabiliana na hali hiyo kampuni ya ACACIA inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu imeamua kujenga kituo kikubwa cha afya kinachogharimu zaidi ya shilingi milioni 800 kwa awamu ya kwanza ikiwa ni moja ya muendelezo wa kusaidia huduma za kijamii kwa vijiji vinavyouzunguuka mgodi huo wa dhahabu ambapo pia kampuni hiyo ya acacia mbali ya kuchangia pato kubwa serikalini wastani wa dola za kimarekani milioni 62 kwa mwaka lakin imekuwa ikishiriki vema miradi ya ujirani mwema katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii katika sekta za elimu,kilimo na maji.

No comments: