Sunday 28 June 2015

Yanga yabanwa Mbavu na Sport club Villa

Mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga wameshindwa kutamba mbele mabingwa wa kombe la FA nchini Uganda timu ya Sports Club Villa baada ya mabingwa hao kulazimishwa sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa hisani ulioandaliwa na taasisi ya Numbani Kwanza kwa ajili ya kuchangia watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi uliomalizika muda mfupi kwenye uwanja wa Taifa.

Winga wa Yanga na timu ya Taifa Simon Msuva alikosa penati baada ya yeye mwenyewe Msuva kufanyiwa madhambi na golikipa wa Sports Club Villa wakati alipopata nafasi ya kwenda kufunga na mwamuzi wa mchezo huo kuamuru ipigwe penati lakini penati hiyo iliota mbawa baada ya Msuva kuipaisha juu.

Mchezo huo kwa upande wa Yanga ulikuwa ni sehehemu ya maandalizi kwa ajili ya michuano ya Kagame ambayo inatarajia kuanza kutimua umbi mapema mwa mwezi Julai ikishirikisha vilabu bingwa vya Afrika Mashariki na Kati.Kipindi cha kwanza kilishuhudiwa kikiwa na upinzani mkali kwa timu zote mbili kufanya mashambulizi kadhaa kwa kupokezana lakini hakuna timu iliyoweza kuweka mpira wavuni kutokana na washambuliaji wa timu zote mbili kushindwa kuzitumia vyema nafasi chache zilizopatikana.

Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Malimi Busungu na nafai yake kuchukuliwa na Kpah Sherman wakati Pato Ngonyani aliingia kuchukua nafasi ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Msuva akaingia kumpokea Amis Tambwe lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia Yanga kuweza kupata bao.

Wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga Deus Kaseke akitokea Mbeya City, Geofrey Mwashiuya aliyekuwa akikipiga Kimondo, na Malimi Busungu kutoka timu ya Mgambo JKT walipata nafasi ya kucheza kwenye mchezo huo na kuonesha viwango vizuri lakini Geofrey Mwashiuya alionekana kukonga nyoyo za mashabiki wengi Yanga waliojitokeza kushuhudia pambano hilo.

No comments: