Friday 24 July 2015

Man City kuvunja benki kumsajili Kevin de Bruyne

Manchester City wanajiandaa ‘kuvunja benki’ kumnasa kiungo mshambuliaji wa Wolfsburg, Kevin de Bruyne, 24.
Mchezaji huyo ameshawaambia klabuni kwamba anataka kuondoka kwenda kucheza Etihad. Matajiri hao wa England wanaingiza dau hilo kubwa baada ya wiki jana tu kumnasa mshambuliaji wa Liverpool, Raheem Sterling kwa pauni milioni 49.
City wanaaminika kuanza na ofa ya pauni milioni 40 lakini inavyoonekana watapanda hadi pauni milioni 60 kumnasa mchezaji ambaye Chelsea waliachana naye wakisema hana kiwango, wakamuuza kwa pauni milioni 18.

Hii itavunja rekodi ya usajili wa wachezaji kwa klabu za England inayoshikiliwa na winga wa Manchester United, Angel Di Maria aliyesajiliwa kwa pauni milioni 59.7 kutoka Real Madrid mwaka jana.
Tena huenda Di Maria akawarahisishia City kumpata De Bruyne, kwani Paris Saint-Germain (PSG) wameachana na mpango wa kumsajili Mbelgiji huyo na badala yake wanamtaka Di Maria.
De Bruyne, 24, awali alitaka kubaki Wolfsburg lakini sasa anasema ana kiu ya kutwaa mataji na City na sasa anatarajiwa kupewa ofa ya mshahara wa £200,000 kwa wiki.
PSG wametoa ofa ya awali ya pauni milioni 45 kwa winga Di Maria mwenye umri wa miaka 27.

No comments: