Thursday 2 July 2015

Risasi za rindima Jiji la mwanza la simama kwa mda

Jiji la Mwanza jana ‘lilisimama’ kwa takriban dakika 10 wakati risasi na mabomu viliporindima kutokana na mapambano kati ya wafanyabiashara ndogondogo na polisi katika mitaa ya Lumumba, Rwagasore, Makoroboi na Barabara ya Nyerere.
Mapambano hayo yalitokea kuanzia saa 5.00 asubuhi baada ya wafanyabiashara hao, maarufu kwa jina la Wamachinga kuamua kutunishiana misuli na polisi waliokuwa kwenye operesheni ya kuwaondoa kwenye mitaa hiyo.
Wamachinga waliokuwa eneo la Hekalu la Wahindi lililopo Mtaa wa Makoroboi, ambalo limekuwa likitawaliwa na vurugu za kila mara baina ya pande hizo na eneo la Stendi ya Tanganyika, waliwatupia mawe polisi waliokuwa kwenye operesheni hiyo na ndipo walipoamua kupambana nao kwa kutumia risasi za moto na mabomu.
Tukio hilo limetokea zikiwa zimepita siku nne tangu Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kumsifia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuwa amepunguza vurugu zilizokuwa zinatokea Mwanza mara kwa mara, akisema siku hizi hawasikii tena purukushani ya polisi, mgambo na wamachinga.
Mwandishi wa Mwananchi ambaye alikuwa karibu na eneo la tukio jana, alishuhudia wamachinga wanaofanya biashara zao wakitoa vitu walivyopanga pembezoni mwa barabara, huku wengine wakikimbia.
Polisi mmoja alishambuliwa na wamachinga hao kabla ya kuokolewa na wenzake.
Wakati polisi wanapiga risasi za moto hewani, wamiliki wa maduka waliyafunga haraka huku wapita njia wakijipenyeza kwenye baadhi ya vichochoro ili kujinusuru.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo alisema walikuwa na operesheni ya kawaida ya kuwaondoa watu wasiofuata utaratibu wa kufanya biashara kwenye maeneo yasiyotakiwa.
Mkumbo alisema baadhi ya wafanyabiashara hao walitaka kuwagomea askari waliokuwa kazini na kwamba, polisi walilazimika kupiga risasi hewani ili kuwatawanya.
“Ni kweli kulikuwa na taharuki, lakini naomba niseme hakukuwa na madhara yoyote na hali hiyo ilitokea baada ya baadhi ya vijana kutaka kujaribu kutunishiana misuli na askari,” alisema Mkumbo na kuongeza:
“Kutokana na vurugu hizo tunawashikilia watu watatu ambao kesho (leo) tutawafikisha mbele ya Mahakama ya Jiji.”
Akihutubia wananchi kwenye viwanja vya Furahisha, Kinana alimsifu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuwezesha kurudisha hali ya utulivu jijini Mwanza.

No comments: