Sunday 26 July 2015

Simba ina wakali watano wapya

wachezaji wa Simba wakiwa kwenye mazoezi
SIMBA ina malengo mengi ya kuyatekeleza katka msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, lakini kubwa zaidi ni usajili hasa wachezaji wa kigeni ambapo imeweka majina ya wachezaji watano mezani ambao wapo kwenye mpango huku ikiwa na nafasi tatu za wazi kwa wachezaji wa aina hiyo.
Simba ina wachezaji wageni wanne ambao wana uhakika nao tayari, hao ni  Simon Sserunkuma, Hamisi Kiiza na Juuko Murshid ambao wote ni raia wa Uganda.Pia inatarajia kumalizana na Laudit Mavugo raia wa Burundi.
 Raphael Kiongera raia wa Kenya yeye ana asilimia kubwa ya kutemwa kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Katika nafasi tatu ilizobakiwa nazo, mpaka sasa majina ya wachezaji Boniface Oluoch na Michael Olunga wote wa Gor Mahia ya Kenya, Emery Namubona wa Vital’O ya Burundi na wengine ni wachezaji kutoka Brazil na Zimbabwe. Hao ndio walioko kwenye faili la Simba na wanaumiza akili wakibishana nani akatwe na nani asajiliwe.
Simba inahitaji kusajili kipa, beki, kiungo na straika ambapo sasa vigogo hao wamefanya mazungumzo na kipa wa Gor Mahia, Oluoch ambaye pia ameonyesha nia ya kukubali na amependekezwa na kocha wa makipa, Idd Salim. Pia Simba ipo kwenye mazungumzo na kiungo kutoka Zimbabwe aliyependekezwa na Kocha Mkuu, Dylan Kerr.
Beki wa Vital’O, Emery tayari alifanya mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo na huenda akatua kwani ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na timu yake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, jana Ijumaa jioni alitarajia kuondoka nchini kwenda Brazili kumfata straika mwingine. Wekundu wa Msimbazi  hao wataziba nafasi ya Kiongera na Emmanuel Okwi ambaye ameuzwa Denmark.
Juzi Poppe alisikika akisema kuwa walikuwa katika mpango wa kuzungumza na Olunga ingawa straika huyo mwenye mabao matatu kwenye michuano ya Kombe la Kagame na 12 kwenye Ligi Kuu Kenya (KPL) amekanusha taarifa hizo na kwamba ana mipango yake.
“Nina mipango yangu, sijaona timu yoyote ikija kuzungumza na mimi juu ya usajili, kikubwa nilichonacho ni kutaka kuisadia timu yangu ifanye vizuri ndani na nje, hivyo mpango huo kwa sasa bado sijaufikiria,” alisema Olunga kauli ambayo iliungwa mkono na kocha msaidizi Frank aliyedai kuwa bado wanahitaji huduma ya straika huyo.
Hata hivyo juzi Alhamis, Rais wa Simba, Evans  Aveva alifafanua akisema: “Olunga hatutamuweza, gharama yake ni kubwa ila tuna mpango na kipa Oluoch na yeye ameonyesha nia ya kuja kwetu.”
Wakati hayo yakiendelea kwa Olunga anayewindwa na timu tatu za jijini Dar es Salaam, Yanga, Simba na Azam, straika wa zamani wa Yanga ambaye anacheza Sofapaka, John Baraza amemshauria Olunga kuwa na subira ili kufanya uamuzi sahihi katika usajili wake.
 Kuna taarifa klabu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini ipo tayari kutoa dola 200,000 sawa na Sh400 milioni kwa Olunga ambaye ana mkataba wa miaka minne na Gor Mahia.
Imeelezwa kwamba Kamati ya Usajili ya Simba kwa sasa haijishughulishi na usajili wa wachezaji wa ndani.
 Wachezaji wapya wazawa waliosajili Simba hivi karibuni ni Peter Mwalyanzi, Mohamed Fhaki, Samir Haji, Musa Hassan ‘Mgosi’ pamoja na Emmanuel Mtumbuka.

No comments: