Thursday 2 July 2015

Wanafunzi 18,751 wakosa nafasi kidato cha tano

Wanafunzi 18,751 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka 2014, wamekosa nafasi ya kujiunga na shule za kidato cha tano kwa sababu mbalimbali ikiwamo ufinyu wa nafasi.
Kati ya hao, wanafunzi 479 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi huku idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo ikiongezeka kwa asilimia 25 kutoka wanafunzi 117 mwaka 2014 mpaka kufikia wanafunzi 147 mwaka huu.
“Baadhi ya wanafunzi wamekosa nafasi kutokana na umri mkubwa na baadhi ya watahiniwa wa kujitegemea wanakosa sifa za kuchaguliwa,” Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema hapa jana alipokuwa akitangaza kuchaguliwa kwa wanafunzi hao.
Alisema wanafunzi 55,003 sawa na asilimia 74.5 ya wanafunzi 73,754 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ndiyo waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano.
Majaliwa alisema kuna ongezeko la ufaulu la wanafunzi 918 mwaka huu, ikilinganishwa na wanafunzi 54,085 waliochaguliwa mwaka 2014 kujiunga na kidato cha tano.
Alisema wanafunzi waliokosa nafasi kuingia kidato cha tano watadahiliwa na Baraza la Taifa la Ufundi (Nacte) kwenye fani mbalimbali kama vile ualimu, afya, maendeleo ya jamii na kilimo.
Alisema ufaulu wa watahiniwa wa kidato cha nne mwaka 2014 kuanzia daraja la ‘distinction’ hadi ‘credit’, yaani ufaulu wa wastani (GPA) wa 5.0 hadi 1.6 ni watahiniwa 73,754 sawa na asilimia 37.4 ya wanafunzi 240,410 waliofanya mtihani huo.
Alisema uchaguzi ulifanyika kwa kufuata machaguo matano ya tahasusi (combinations) yaliyojazwa na wanafunzi kwenye fomu ya uchaguzi ‘Selform.’
Alisema mfumo wa kompyuta ulitumika katika kumpanga mwanafunzi katika uchaguzi wake wa masomo na shule kwa kuanzia na chaguo la kwanza. “Kama mwanafunzi atakuwa hana sifa katika machaguo yote aliyoomba, hupangiwa chaguo la somo alilofaulu zaidi na katika shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi kulingana na tahasusi na nafasi zilizopo,” alisema Majaliwa.
Alisema wanafunzi 29,744 watajiunga na masomo ya sayansi na 25,259 watajiunga na masomo ya sanaa na biashara.
Aliwataka wanafunzi waliochaguliwa kuripoti katika shule walizopangiwa ili kuanza muhula wa kwanza wa masomo unaotarajiwa kuanza Julai 18.
“Naagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya wiki mbili kuanzia tarehe ya mwisho ya kuripoti, nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi,” alisema Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, Lindi.
Aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kila tarafa kuwa na shule ya kidato cha tano inatekelezwa kikamilifu ili kuwezesha wanafunzi wote wanaofaulu kupata nafasi ya kuendelea na masomo. “Wadau wote wa elimu pia wahakikishe kuwa shule zote zinazoanzishwa kwa ajili ya kidato cha tano zinakuwa na mabweni kwa kuwa shule hizi ni za kitaifa na zinapokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini,” alisema.
Kutokana na kuongezeka kwa ufaulu katika masomo ya sayansi, Majaliwa alihimiza shule za kidato cha tano zinazoanzishwa kuwa na maabara ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa tahasusi za sayansi na kukidhi mahitaji ya shule husika.
 CHANZO: MWANANCHI

No comments: