Saturday 25 July 2015

Yanga kwa raha zao watinga robo fainali kagame Cup

Deus Kaseke akiwatoka wachezaji wa KMKM
YANGA jana ilitinga robo fainali ya Kombe la Kagame baada ya kupata ushindi wa pili mfululizo kwa kuizamisha KMKM ya Zanzibar kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ushindi huo umewafanya mabingwa hao wa Tanzania Bara kufikisha pointi sita, pointi moja nyuma ya timu mbili za Al Khartoum ya Jamhuri ya Sudan na Gor Mahia ya Kenya zinazoongoza Kundi A.
Yanga ilianza kwa kufungwa mabao 2-1 na Gor Mahia wiki moja iliyopita, lakini Jumatano wiki hii ilizinduka na kuichapa Telecom ya Djibouti mabao 3-0, na hivyo kufufua matumaini ya kusonga mbele.
Kwa matokeo ya jana, Al Khartoum na Gor Mahia ambazo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza jana kwenye uwanja huo, zinaungana na Yanga kucheza robo fainali wakati KMKM imetupwa nje sawa na Telecom.

Kundi hilo la A lenye timu tano, linatoa timu tatu kucheza robo fainali wakati makundi ya B na C yenye timu nne yatatoa timu mbili kila moja na kutakuwa na timu bora moja kufanya idadi ya timu nane za robo fainali.
KMKM imemaliza mechi zake jana kwa kufikisha pointi tatu baada ya kuishinda Telecom bao 1-0 katika ufunguzi, lakini ikafuatiwa na vipigo vya mabao 3-1 kutoka kwa Gor Mahia na mabao 2-1 kutoka kwa Al Khartoum.
Mabao ya Yanga jana, ambayo yote yalipatikana katika kipindi cha pili, yalifungwa na Malimi Busungu ambaye amefikisha mabao matatu sawa na Michael Olunga wa Gor Mahia, na jingine lilifungwa na beki wa KMKM.
Busungu alifunga bao lake kwa kichwa baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa KMKM, huku awali akifaidika na pasi ya Donald Ngoma, wakati beki wa KMKM, Khamis Ali Khamis alijifunga alipojaribu kuokoa mpira wa Amissi Tambwe, lakini akaupiga kichwa kilichompita kipa wake Nassoro Abdulla Nassoro.
KMKM kama ilivyokuwa katika mechi zilizopita, ilionekana kuhimili vishindo katika dakika za mwanzo, lakini kadri muda ulivyokwenda, ilionekana kukata pumzi na kuruhusu mashambulizi zaidi langoni mwao.
Aidha, Yanga ilibadilika jana ikipumzisha wachezaji wake nyota kadhaa akiwamo mfungaji wake nyota, Simon Msuva na Kpah Sherman ambaye taarifa inasema kwamba ameuzwa kwa klabu ya Afrika Kusini, huku ikimweka benchi Tambwe kabla ya kuingia kipindi cha pili kumbadili Busungu.
Lakini Ngoma ambaye hakucheza mechi iliyopita baada ya kuoneshwa kadi nyekundu katika mechi ya kwanza dhidi ya Gor Mahia, alikuwa mwiba mchungu sana kwa KMKM na alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Yanga itamaliza mechi zake kesho kwa kucheza na Al Khartoum wakati Gor Mahia itamaliza na Telecom. Leo, mabingwa wa zamani wa Tanzania Bara, Azam FC ambayo inaongoza Kundi C ikiwa na pointi sita, itacheza na Adama City ya Ethiopia na KCCA ya Uganda itavaana na Malakia ya Sudan Kusini, zote zikiwa na pointi tatu.

No comments: