Wednesday 11 November 2015

Buhari atangaza baraza lake la mawaziri

AdeosunBi Adeosun ameteuliwa waziri wa fedha
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari hatimaye ametangaza wizara na mawaziri watakaozisimamia, miezi saba baada yake kushinda uchaguzi wa urais.
Nafasi muhimu ya waziri wa fedha ameikabidhi mwanauchumi Kemi Adeosun, aliyesomea Uingereza kabla ya kurejea Nigeria na kuhudumu kama kamishna ya fedha jimbo la Ogun.
Jenerali mstaafu Mansur Dan Ali atakuwa Waziri wa Ulinzi, na kazi yake kuu itakuwa kuongoza vita dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.
Gavana wa zamani wa jimbo la Lagos Babatunde Fashola ameteuliwa waziri wa kawi, ujenzi na makazi na anakabiliwa na kibarua cha kutatua mzozo wa umeme Nigeria.
Mwanasiasa mkongwe ambaye pia ni mkulima Audu Ogbe ameteuliwa waziri wa kilimo.
Nigeria ina ardhi kubwa ambayo ikutumiwa vyema inaweza kubuni nafasi za kazi na kupunguza utegemezi wa mafuta, wadadisi wanasema.
Kuzinduliwa kwa baraza hilo lenye mawaziri 36 kumefanyika miezi saba baada ya uchaguzi wa urais.
Buhari
Buhari alishinda uchaguzi uliofanyika Machi
Bw Buhari aliyechaguliwa Machi alikuwa ameahidi kukabiliana na ufisadi na ukosefu wa usalama, na aliahidi kuteua watu wenye ujuzi na wasio na ila.
Mhariri wa BBC Hausa Mansur Liman anasema baraza hilo la Rais Buhari litashangaza watu na hasa uteuzi wa Bi Adeosun kuwa waziri wa fedha. Wengi walitarajia Okechukwu Enelemah, aliyeteuliwa waziri wa biashara na uwekezaji, angeteuliwa waziri wa fedha.
Rais Buhari pia ameshangaza wengi kwa kumteua mkuu wa zamani wa jeshi Jenerali Abdurrahman Dambazau kuwa waziri wa mambo ya ndani. Wengi walitarajia angeteuliwa waziri wa ulinzi.
Amina Mohammed, mshauri wa zamani wa mkuu UN Ban Ki-Moon kuhusu maendeleo endelevu, alitarajiwa kuteuliwa waziri wa mipango lakini ameteuliwa waziri wa mazingira.

No comments: