Saturday 6 February 2016

Balozi wa Tanzania aridhishwa na hali Bangalore

Kijazi
Balozi Kijazi amesema wenyeji na Waafrika wanafaa kuwa wakikutana na kujadiliana

Balozi wa Tanzania nchini India John Kijazi amesema ameridhika kwamba serikali ya nchi hiyo imeweka mikakati ya kutosha kuwalinda wanafunzi, kufuatia kisa ambapo wanafunzi wanne walishambuliwa mjini Bangalore Jumapili.
Akizungumza baada ya kutembelea pahala ambapo wanafunzi hao walishambuliwa, na mmoja wao kuvuliwa nguo, Bw Kijazi amesema huenda kisa hicho kilitokana na suitafahamu.
“Kilicho muhimu ni tuangalie siku za usoni kwa sababu tusipofanya hivyo tutapotea. Tunahitaji kutatua tatizo la sasa lakini pia tuangalie mikakati ya muda mrefu,” ameambia wanahabari.
“Nimeridhishwa na hatua za kiusalama ambazo zimechukuliwa na serikali hapa. Kuna maafisa ambao wamesimamishwa kazi.”
Balozi huyo alikata kutaja kisa hicho kama cha ubaguzi wa rangi.
“Hatukutaka kuangazia masuala ya ubaguzi wa rangi na mambo mengine kwa sababu nadhani vyombo vya habari vinapendezwa sana na hilo. Tumejadiliana kuhusu masuala halisi na hatua madhubuti ambazo tayari zimechukuliwa na serikali ya hapa,” amesema.
Bw Kijazi alisafiri hadi Bangalore akiandamana na maafisa wawili wa wizara ya mambo ya nje ya India ambapo walikutana na waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Karnataka Dkt G Parameshwara na wakuu wa polisi wa jimbo hilo.
Polisi mjini Bangalore wamewakamata watu tisa kuhusiana na kisa hicho.
Mkuu wa kituo cha polisi cha Soldevenahalli pia amesimamishwa kazi kwa tuhuma kwamba hakuchunguza kwa undani kisa hicho baada ya mmoja wa wanafunzi hao kupiga ripoti.
Konstebo wa polisi pia amesimamishwa kazi kwa kutochukua hatua kuzuia wanafunzi hao wasishambuliwe na umati.

No comments: