Monday 21 March 2016

Barack Obama wa Marekani aliwasili Cuba Jumapili katika ziara ya kihistoria

Rais Obama akipunga mkono mara baada ya kuwasili HavanaHAVANA - Rais Barack Obama wa Marekani aliwasili Cuba Jumapili katika ziara ya kihistoria, huku mataifa haya mawili yakiendelea na hatua za kurejesha uhusiano wao baada ya kufarakana kwa miaka 55.
Obama, rais wa kwanza wa Marekani aliye madarakani kutembelea Cuba katika miaka karibu 90, atakamilisha ziara yake kwa hotuba ya moja kwa moja kwa watu wa Cuba akielezea dira yake ya uhusiano wa baadaye baina ya Marekani na Cuba.
Obama alishuka kutoka katika Air Force One huku kukiwa na kiwingu na mvua za rasharasha katika uwanja wa Havana kiasi cha saa kumi na nusu jioni Jumapili.

Obama aliandamana na ujumbe unaojumuisha wabunge kutoka vyama vyote vya siasa Marekani, wakuu wa mashirika na Wamarekani mashuhuri wenye asili ya Cuba. Aidha anaandamana na familia yaka, akiwemo mkewe Michelle, watoto wao wawili, Malia na Sasha na mama mkwe, Marian Robinson.
Katika hotuba yake katika Hoteli ya Melia Habana, Rais Obama alisema, "Kuwa na ubalozi wa Marekani Cuba ina maana tuna uwezo wa kushirikiana vizuri katika thamini zetu, maslahi yetu na kufahamu zaidi" maswala waliyonayo Wacuba. "Hii ni ziara ya kihistoria na fursa ya kihistoria."
Rais Obama na familia yake pia walitembelea mji mkongwe wa Havana pamoja na kanisa kuu la mji huo huku kukiwa na mvua kali. Baadaye walipata chakula cha usiku katika mkahawa wa San Cristobal. Makundi ya watu walijazana kuona msafara wa Obama wakati unapita katika mitaa myembamba ya Havana.
Ikulu ya Marekani - White House - inasema ziara hiyo ni ishara ya mwanzo mpya katika uhusiano baina ya nchi hizi zilizokuwa mahasimu wakati wa vita vya itikadi.

No comments: