Thursday 14 April 2016

Video ya Boko Haram yaonesha wasichana wa Chibok

WasichanaWanachama wa vuguvugu la Bring Back Our Girls waliandamana mjini Lagos Jumatano kutetea kuachiliwa kwa wasichana hao
Kanda ya video iliyotumwa kwa maafisa wa serikali ya Nigeria kutoka kwa kundi la wapiganaji wa Boko Haram inaonesha baadhi ya wasichana waliotekwa eneo la Chibok wako hai.
Ni miaka miwili tangu kutekwa kwa wasichana 276 kutoka shule moja katika mji wa Chibok.
Ni wasichana 15 wanaoonekana kwenye kanda hiyo ya video ambayo inaaminika ilipigwa Siku ya Krismasi.
Video hiyo imepeperushwa hewani na shirika la utangazaji la marekani la CNN.

Maafisa wa Nigeria wamesema mashauriano kati ya serikali na wapiganaji hao wa Kiislamu yanaendelea lakini yatasalia kuwa siri kwa sababu za kiusalama na ili kuzuia wanaofanikisha wazungumzo hayo wasitambulike.
Mama
Mamake mmoja wa wasichana waliotekwa
Mwandishi wa BBC aliyeko Abuja anasema video hiyo imewapa matumaini baadhi ya raia wa Nigeria kwa sababu inaonesha baadhi ya wasichana wako hai.
Lakini baadhi wanasema hali kwamba ni wasichana wachache sana waliooneshwa kwenye video hiyo inaibua wasiwasi kuhusu hatima ya wasichana hao wengine walioonekana kwenye video hiyo.
Kanda hiyo ya video ndiyo ya kwanza kutolewa ikiwaonesha wasichana hao tangu mwezi Mei mwaka 2014.
Serikali ya Nigeria imekosolewa kwa kushindwa kuwakomboa wasichana hao.
Chibok Shule ya Chibok inapatikana jimbo la Borno
Kwa muda mrefu, kitambulisha mada #BringBackOurGirls (Turejeshee wasichana wetu) kilivuma sana mtandao wa Twitter.
Mke wa Rais wa Marekani Michelle Obama ni mmoja wa watu mashuhuri walioshiriki katika kampeni ya kupigania kukombolewa kwa wasichana hao

No comments: