Thursday 16 February 2017

Kichanga atupwa, wapita njia wamuokoa

Mtoto aliyetupwa na kuokotwa akiwa katika Hospitali teule ya wilaya ya Mbeya Ifisi, Mbalizi Mbeya.

Sauti ya kilio cha kichanga wa kiume aliyekuwa ametupwa na mamaye asiyefahamika, kimeliondoa giza na kuwashitua wapita njia ambao wamemuokota akiwa hai.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema jana majira ya usiku wa saa tatu usiku kukiwa na baridi, walisikia sauti ya kulia kichanga mita 100 kutoka katika kilabu cha pombe za kienyeji cha Kango kata ya Nsalala Mbalizi Mbeya Vijijini.
Wamesema waliposogea walimkuta mtoto huyo wa kiume akiwa ameviringishwa (visepe), katikati ya nyasi Jirani na Nyumba ambayo haikaliwi na mtu.
Baadae walimpeleka kituo cha Polisi Mbalizi ambako walipata msaada wa gari binafsi baada ya askari waliokuwepo kituoni kuwaambia kuwa gari la serikali halikuwa na mafuta.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni mwanakikundi cha Taarifa na Maarifa kata ya Nsalala, Tausi Sanga alisema baada ya kumkuta mtoto huyo alihusika kumpeleka hospitali teule ya wilaya hiyo Ifisi.
"Tulipomfikisha Polisi na kuambiwa hawana mafuta kwenye gari hatukupendezwa lakini kuna askari ni Trafiki akampigia mwenzake simu akaja kutuchukua na gari yake binafsi na kutuleta hospitalini" alisema Tausi alipokuwa na wanakikundi wenzake katika hospitali ya Ifisi.
Muuguzi mkuu wa Hospitali hiyo Elmath Sanga alisema mtoto huyo anaendelea vizuri na kuna muuguzi anamuhudumia kwa karibu ikiwemo kumpatia maziwa.
"Hitaji kubwa la sasa ni nguo" alisema Muuguzi huyo mbele ya Mwandishi wa habari na wanaharakati hao wa kikundi cha Taarifa na Maarifa.
Baadhi ya wanakikundi cha Taarifa na maarifa kata ya Nsalala Mbalizi Mbeya, wakiwa nje ya Hospitali teule ya wilaya ya Mbeya baada ya kutoka kumuona mtoto waliyeshiriki kumuokota jana usiku na kumfikisha kituo cha Polisi Mbalizi kisha hospotalini hapo.

No comments: