Saturday 1 April 2017

MADIWANI DODOMA WAMFUNGIA MKURUGENZI OFISINI

KAMATI ya Uongozi, Mipango na Fedha ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma, ilifunga Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mohamed Maje ikidai ameshiNdwa kutekeleza maelekezo ya madiwani. 
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dornart Nghwezi alisema Mkurugenzi huyo na timu yake wamekuwa hawatekelezi kwa wakati maelekezo ya Baraza hali inayosababisha kuwapo malumbano ya mara kwa mara yanayokwamisha maendeleo. 

Alisema wamewahi kutoa tamko la baraza la kutokuwa na imani na mkurugenzi huyo kwa kushindwa kusimamia mapato na shughuli za Halmashauri. 
Aidha, alisema katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Machi 16, mwaka huu, kikao cha Kamti ya Uongozi, Mipango na Fedha walipanga kufanya kikao kingine Machi 27, lakini walipofika ofisini hawakukuta makabrasha pamoja na uwepo wa kikao na walipojaribu kumpigia simu, Mkurugenzi huyo hakupatikana. 
Maje alikiri kuzuiwa kuingia ndani ya ofisi na madiwani hao walioongeza kufuri lingine nje ya geti la nje la ofisi. Alisema hali hiyo ilimlazimu kutoa taarifa Polisi na uongozi wa wilaya. 
Maje alisema ni kweli walipanga kufanya kikao hicho Machi 27, lakini kikaathiriwa na ugeni wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uongozi na Serikali za Mitaa ambao ulitaka kutembelea miradi mbalimbali ya halmashauri hiyo. 
“Ni kweli jana (juzi) kulitakiwa tuwe na kikao lakini kuna ugeni wa Kamati ya Bunge ya kutembelea halmashauri yetu ikiwa ni pamoja na wakuu wa idara wengi walitakiwa kwenda kwe ziara hiyo sasa hicho kikao angekifanya nani? Tulimpa taarifa Mwenyekiti sasa sielewi kwanini waliamua kufanya hivyo,” alisema Mkurugenzi huyo. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri alisema kilichofanywa na madiwani hao hakikuwa sahihi kwa kujaribu kumzuia kuingia ofisini. 
Alisema kufunga milango ya ofis ni kitendo cha kijinai lazima taratibu, kanuni na sheria zifuatwe.

No comments: